Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omar Ali Omar

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Wete

Primary Question

MHE. OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:- Je ni kwa nini askari polisi wasiwekewe utaratibu wa kusamehewa kodi katika vifaa vya ujenzi na kupewa viwanja kwa bei elekezi ili wawe na moyo wa kulitumikia Taifa bila kujiingiza katika njia za udanganyifu kwa lengo la kujiandaa na maisha baada ya kustaafu?

Supplementary Question 1

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba posho ya shilingi 100,000 ambayo ilikuwa inatolewa kwa ajili ya kuwawezesha askari wetu waweze kukidhi haja ya kuweza kujenga, tukiangalia kwa mtazamo ni kwamba posho hiyo ilikuwa ni ndogo na hata askari wakipewa miaka 100 hawawezi kufanya ujenzi kwa posho hiyo.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwawezesha askari wetu kuwaongezea posho hii ili iendane na utaratibu wa kuweza kujenga kwa askari wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili; je, sasa Serikali haioni kwamba kuna haja kwa Wizara kuhakikisha kuona kwamba pamoja na kwamba askari wetu wanaintelijensia ya hali ya juu, hatuoni sasa kwamba kuna haja sasa ya ule utaratibu wa mwanzo kuweza kutumika ili kwamba askari wetu tuweze kuwaweke katika mazingira mazuri waweze kulinda nchi hii, raia pamoja na mali zao? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari ama ina utaratibu gani sasa wa kuongeza hii posho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo dhamira kwa sababu kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba vyombo vyetu vya ulinzi hasa Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri na kwa kweli tunayo kila sababu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuendelea kufanya kazi vizuri, katika hili tunawapongeza sana. Kikubwa ni kwamba utaratibu wa kuongeza hizi posho upo, tumeshaupanga/tumeshaufikiria maana hata katika bajeti ambayo tuliiwasilisha juzi tulilizungumza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa awe na stahamala kwa sababu hii mipango inahitaji fedha na tupo mbioni kuhakikisha kwamba tunatafuta hizo fedha ili tuweze kuwaongezea kwa sababu hatuwezi tukasema kwamba kesho tutawaongezea, kwa hiyo, kesho watazipata lakini the way ambavyo kasungura ketu kananenepa ndivyo ambavyo tutakapokuwa tunawaongezea na wao hii posho ili sasa waendelee kufanya kazi nzuri zaidi ya kulinda raia na mali zao. Kwa hiyo, hiyo nia ya kuwaongezea posho ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, hakuna haja ya kurejesha ule utaratibu wa mwanzo, mimi nadhani Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tuende tukakae na wenzetu tukalifikirie hili, tukapange halafu tutaona sasa namna bora ya kuboresha haya mambo ili sasa kuweza kurejesha ule utaratibu wa mwanzo ambao kama yeye Mheshimiwa Mbunge ameuzungumzia. Nakushukuru. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Khamis, lakini nataka nikubaliane na muuliza swali la msingi Mheshimiwa Lambert pamoja na maswali yake ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni kweli tunakubaliana kwamba vijana hawa askari polisi wanafanya kazi nzuri kwa nchi na Taifa lao na pengine wanafanya hivyo katika mazingira magumu na wengine kulingana na vyeo vyao ni vigumu sana kujikomboa na kupata hata maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lililosemwa katika swali la msingi ni kama je, Serikali haioni haja ya kuwapatia vijana hawa viwanja kwa bei nafuu? Nataka niseme sisi kama Wizara tunalichukua hili, tutajadiliana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone uwezekano huo kwa sababu ni jambo jema kabisa na wengine kweli wanamaliza/wanastaafu wakiwa kwanza na umri mdogo kulingana na Kariba ya ajira yenyewe ya Jeshi la Polisi, mtu ana miaka 54 anastaafu, halafu hana hata nyumba wala kiwanja. Nataka nikubaliane kwamba acha tulifanyie kazi, tuone kwa mfumo ambao uliopo kama tunaweza tukawapatia vijana hawa angalau viwanja, angalau kwa wale wa vyeo fulani fulani ambao unajua wapo kidogo underprivileged. Nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri, mmezungumzia upande wa viwanja nafikiri pia Serikali mtajipanga na hoja ya pili ya muuliza swali ameuliza mambo mawili; msamaha wa kodi katika vifaa vya ujenzi pamoja na viwanja kwa bei elekezi. Kwa hiyo, nafikiri…, karibu.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa na utaratibu wa duty free shops kwa ajili ya hawa askari. Maduka haya yalitumika na ukatokea ukiukwaji mkubwa sana wa taratibu za kikodi na kutokana na mazingira hayo mambo mengi mabaya yalitokea, Serikali ikaona bora kuondoa ile kwa sababu waliokuwa wananufaika ni watu fulani, fulani tu hata walengwa pengine walikuwa hawanufaiki, tukaona bora waingiziwe fedha zao na kwa utaratibu wa sasa wanalipwa shilingi 300,000 kila baada ya miezi mitatu, ni kitu fulani kuliko wengine ambao walikuwa vijijini huko hata duty free shops hizo hawazioni. Na utaratibu huo wa ku-institutionalize leo ni vigumu sana. Kwa hiyo, utaratibu wa fedha kuingizwa kwenye akaunti zao umekuwa ni bora na wanaufurahia sana. (Makofi)