Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Malangali ndani ya Wilaya ya Wanging‟ombe na wafanyakazi wa Hifadhi ya Mpanga?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kwa muda mrefu sana kumekuwepo mgogoro wa wananchi na Serikali kwa maana ya Hifadhi za Serikali na wananchi wamekuwa wakilalamika sana kwa sababu watu wameongezeka lakini ardhi haiongezeki:-
Je, ni lini sasa Serikali italeta sheria Bungeni ili ifanyiwe marekebisho kuweza kumaliza mgogoro baina ya wananchi na Serikali?
Swali la pili, kwa kuwa kuna mgogoro mkubwa na wa muda mrefu katika Hifadhi ya Pori la Kagerankanda na Serikali; na wananchi wamekuwa wakipata shida sana kutokana na shida iliyopo kwa sababu kwa muda mrefu hifadhi haijafanyiwa marekebisho ya kupimwa mipaka:-
Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri tutafuatana kuja Kasulu kwa ajili ya kumaliza suala la Mipaka katika Wilaya ya Kasulu katika eneo la Kagerankanda?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ametaka kujua ni lini Serikali italeta sheria ambayo itakwenda kumaliza migogoro kati ya Serikali na Wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, mgogoro uliopo pengine unaweza kuwa umchangiwa pia na baadhi ya watumishi wetu, kwa sababu 2002 mhifadhi aliyekuwa katika ile mbuga alikwenda akabainisha mipaka ambayo ilikosewa, matokeo yake ikabidi warudie tena 2009 baada ya mhifadhi mwingine kubadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mhifadhi alipobadilisha tena naye mgogoro ukawa mkubwa zaidi. Ndiyo maana hapa sasa Serikali ilibidi iingilie kati katika kuangalia ile GN iliyokuwepo na kuweza kujua mipaka halisi ni ipi. Kwa sababu mgogoro umekuwa mkubwa zaidi, ndiyo maana pia Mkuu wa Wilaya ya Wanging‟ombe akaunda Tume kwa ajili ya kutaka kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimelizungumza hili la mipaka kwamba lina matatizo, tutakwenda kushirikiana Wizara zinazohusika kwa sababu huu mgogoro hauhitaji kutungiwa Sheria, ni namna tu ya kutafsiri mipaka katika eneo ambalo lina mgogoro. Wananchi wanadai wako nje, lakini mipaka ya hifadhi, wahifadhi wanasema wako ndani ya hifadhi. Ndiyo maana nimesema, hapa tutakaa Wizara yangu ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalalii ili tumalize huo mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameongelea pori la Kagerankanda; nalo lina mgogoro na wananchi na akataka tuongozane kwenda Kasulu kwa ajili ya utatuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya kikao hiki cha Bunge na baada ya kukutana Wizara zote zinazohusika na migogoro hiyo kama ambavyo imewasilishwa na Waheshimiwa wabunge na siyo huu mgogoro wa Kasulu tu na migogoro mingine, tutapanga ratiba maalum ya kufika katika maeneo ili tuweze kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa ni kujua chanzo cha mgogoro: Je, ni Wizara inatakiwa kwenda na Wizara nyingine au uko kwenye mipaka kwa maana ya TAMISEMI au ni hifadhi pamoja na ardhi ili tuweze kujua?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukishabainisha kwa sababu orodha tunayo kwa Majimbo yote au kwa nchi nzima, basi tutatatua kulingana na nature ya mgogoro wenyewe.