Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Haji Khatib Kai

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Micheweni

Primary Question

MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:- Tanzania ni mwenyeji mkubwa kati ya nchi zilizounda Umoja wa Afrika Mashariki, hivyo basi, hupelekea au hupaswa Watanzania kufaidika na soko la Afrika Mashariki:- (a) Je, Serikali inawashauri nini wananchi wake wanapokwenda kibiashara kwenye nchi zinazounda umoja huo? (b) Je, pindi wanapopata matatizo au vikwazo katika nchi husika ni wapi watapeleka malalamiko?

Supplementary Question 1

MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kupata maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imeshauri wananchi kuzitambua na kuzitumia fursa za soko la Afrika Mashariki na kwa kuwa Serikali na Wizara husika, ina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania kuhusiana na soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Ni kwa nini na ni lini Serikali au Wizara husika itatoa elimu kwa wananchi wa Kaskazini Pemba hasa Jimbo langu la Micheweni ili waepukane na tabu ambazo wamekuwa wakizipata kila mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, endapo matatizo yatatokea au vikwazo vitatokea wananchi wawasiliane na Wizara yake au Balozi zetu. Binafsi wananchi hawa au Watanzania hawa wapatao 130 wanaotoka Jimbo langu na Majimbo mengine, waliposhikwa nchini Kenya waliwasiliana na mimi na mimi nikawasiliana na Balozi zetu zote mbili Nairobi na Mombasa kwa ajili ya msaada, msaada ambao ulishindikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifuata utaratibu wa kwenda Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa msaada zaidi na nilikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na tulikubaliana kilichofanyika si sahihi. Kwa bahati mbaya, naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri, hadi sasa sijapata mrejesho wowote, je, atakubaliana nami kwamba Watanzania hawa ambao hawakupata msaada si ni wazi kwamba, kutokana na itikadi yao ya kisiasa ndilo jambo ambalo lilipelekea kushindwa kupatikana msaada wowote? (Makofi)

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Ningependa nimjibu Mheshimiwa Kai, Mbunge wa Micheweni maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine kwa upande wa Tanzania nimekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kwa mwaka mzima. Hili suala analolieleza hapa ndiyo nalisikia kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge hilo analolisema ni kitu kizito sana, itabidi tukae chini na Wizara husika tuweze kuelewa kilitokea kitu gani hata kama alikwenda Ubalozi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi, naomba kutoa wito kwa wananchi wa Tanzania wanaofanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukipata matatizo kama Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu la swali la msingi, hakikisha unakwenda Ubalozi, ukishindwa nenda Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ukishindwa nenda TCCIA (Tanzania Chamber of Commerce and Industrial and Agriculture), ukishindwa nenda Tanzania Exporters Association (TEA).
Kwa hiyo, taasisi zote hizi zitakusikiliza lakini hakikisha Wizara inapata taarifa kwa sababu tuna miundombinu tayari ya kulalamika.Wenzetu wanajua sana kulalamika, Watanzania tunalalamika chini kwa chini.
La pili, lini tutatoa elimu kwenye Jimbo lake? Elimu tunatoa kuanzia hii Wizara ilipoanzishwa, tunatoa kupitia vipindi vya redio, television, pamphlets, kupitia mikutano, hatuwezi kufanya specifically kwa Jimbo moja, lakini naomba niwahakikishie Watanzania kwamba biashara Afrika Mashariki sasa hivi imeongezeka kwa kasi na Watanzania tunachangia kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa wafanyabiashara wa Kitanzania, tutumie hii fursa ya kupeleka bidhaa katika nchi za Afrika Mashariki kwenye bei nzuri, hulipi chochote kwa bidhaa zote ambazo zina uasilia wa Afrika Mashariki, unachotakiwa tu ni kupata hiyo certificate ya origin pale unapofika mpakani hasa kama bidhaa yako haizidi dola 2,000 na kwa wafanyabiashara wakubwa wao wanapata kutoka TCCIA.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:- Tanzania ni mwenyeji mkubwa kati ya nchi zilizounda Umoja wa Afrika Mashariki, hivyo basi, hupelekea au hupaswa Watanzania kufaidika na soko la Afrika Mashariki:- (a) Je, Serikali inawashauri nini wananchi wake wanapokwenda kibiashara kwenye nchi zinazounda umoja huo? (b) Je, pindi wanapopata matatizo au vikwazo katika nchi husika ni wapi watapeleka malalamiko?

Supplementary Question 2

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametuelekeza Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza katika Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Jimbo la Vunjo ni sehemu ya kuchangamkia fursa hizo especially eneo la Taveta. Sasa lini Serikali itaharakisha ujengaji wa soko la Kimataifa la Lokolova pale Himo ili fursa hizo ziweze kutumika kwa Watanzania?

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa soko la analolieleza Mheshimiwa Mbatia ni moja tu ya miradi mingi ambayo Serikali imefanya kuongeza fursa ya Watanzania kushiriki katika biashara ya Afrika Mashariki. Yeye mwenyewe atakuwa ni shahidi kwamba Serikali sasa hivi ina miradi ambayo nusu yake imekamilika ya kujenga vituo vya pamoja kwenye mipaka vinane, tunaita one stop boarder post na tumejenga vituo vizuri sana ambavyo vimeharakisha biashara katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile analolisema Mheshimiwa Mbatia ni suala ambalo tunafikiri ni muhimu kwa Wizara sasa hivi ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa maeneo yote ya mipakani, kwa kweli tuharakishe kumalizia miradi yote ambayo tumeianza na ambayo tunaifikiria ya masoko ya pamoja kwa sababu wenzetu upande wa pili wamechangamkia kweli fursa hiyo. Nadhani huo ni wajibu wa Serikali kuliangalia hilo kwa makini kwa kila mpaka siyo tu kwenye Jimbo la Vunjo.