Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:- Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye matumaini, hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la maji ni sugu katika Kata ya Saja, Kijombe, Wanging‟ombe na Njombe Mjini, je, Serikali itatatua lini tatizo hili nimekuwa nikiulizia mara kwa mara swali hili katika Bunge lililopita? (Makofi)

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niongezee kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya kama ifuatavyo:-
Kwanza tunakiri kweli kuna upungufu mkubwa wa maji maeneo hayo unayoyataja, Njombe Mjini kuna tatizo kubwa, Makambako kuna tatizo kubwa, hizo Kata za Saja, Kijombe na Wanging‟ombe zote zina matatizo makubwa. Ndiyo maana Serikali imeshafanya usanifu wa kukarabati miradi iliyopo na kuongeza miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imepata milioni 500 US dollar sawasawa na shilingi za Kitanzania trilioni moja kwa ajili ya kuweza kukarabati miradi pamoja na Miji mingine 17. Kwa hiyo, kazi hii tuko kwenye hatua ya mwisho ya kuanza kutekeleza na tutafanya hivyo kwa kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana wananchi wa huko wawe na imani na Serikali ya Awamu ya Tano kwamba tunakwenda kumaliza tatizo hili. Mheshimiwa Rais alipokuwa Makambako, nakumbuka kabisa alisema nipeni Urais, nitakwenda kumaliza tatizo la maji Makambako. Mheshimiwa Sanga alikuwepo nataka nikuhakikishie tatizo la maji Makambako tunakwenda kulimaliza. Ahsante. (Makofi)

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:- Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 2

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, vilevile niishukuru kauli ya Serikali kwa kunipa matumaini kwamba sasa wananchi wangu wangu wa Makambako watapona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Makambako ni la muda mrefu takribani zaidi ya miaka 30 na kitu, mradi ambao tunao pale ulikuwa unahudumia watu 15,000 na sasa tumeshaongezeka na tumefikia zaidi ya watu 160,000. Je, Serikali imejipangaje kuona sasa tatizo hili linatatuliwa mapema na kama Rais alivyokuja alituahidi kwamba tatizo hili atalitatua?
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Waziri mwenye dhamana alikuwepo siku ile wakati Rais anazungumza kwamba, atakapomteua Waziri aanzie Makambako leo unawaambiaje watu wa Makambako?
La pili…

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotoa maelezo ya nyongeza kwa muuliza swali la msingi niseme tu kwamba, nitakachofanya sasa baada ya Bunge hili mimi nitatembelea Makambako, tutakwenda kuongea na wananchi ili tuwape mpango ambao tunao wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:- Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 3

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo la maji la Makambako kwa asilimia kubwa linafanana na Jimbo la Bunda Mjini. Natambua Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mradi mkubwa wa maji tangu mwaka 2006 ni wa muda mrefu sana na ulikuwa ukamilike, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika.
Mheshimiwa Naibu spika, mradi ule unaanzia Kata ya Guta lakini hauna vituo na kama mradi ule wa kupeleka maji katika Mji wa Bunda ukiwa na vituo, vile vijiji jirani Kinyambwiga, Tairo, Guta A, Guta B, Gwishugwamala, vyote vitanufaika na mradi wa maji. Sasa je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kuweka vituo ili vijiji hivyo vinavyopita mradi kwenda Mji wa Bunda vinufaike na mradi huo? (Makofi)

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna mradi ambao tumetekeleza katika Mji wa Bunda tumeweza kujenga bomba kubwa kutoka Ziwa Victoria, tumeweza kujenga matanki, hiyo ni awamu ya kwanza. Sasa awamu ya pili tutakwenda kusambaza katika maeneo yale ambayo bomba hilo limepita. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba, kazi hiyo tutakwenda kuifanya kwa manufaa ya wananchi wa Bunda. Ahsante. (Makofi)

Name

Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:- Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 4

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Wilaya ya Mvomero ipo miradi ya maji iliyo chini ya Wizara katika maeneo ya Tarafa za Mgeta, Mlali, Turiani na Mvomero na kwa kuwa miradi hiyo imeanza, lakini bado haijakamilika na kwa kuwa Serikali imeshatumia mamilioni ya fedha. Je, Serikali sasa iko tayari kuleta fedha zilizobaki ili miradi ikamilike katika maeneo hayo na wananchi wapate maji safi na salama Wilayani Mvomero?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, jana kwenye jibu la msingi la matatizo ya maji nilieleza katika awamu ya kwanza ya programu ya maji iliyoanza mwaka 2007 na imeishia mwaka 2012 tulikuwa na miradi 1,855.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi iliyokamilika ni miradi 1,143 na miradi inayoendelea ni miradi 454 ambapo katika hii miradi inayoendelea ipo miradi katika Jimbo la Mheshimiwa Saddiq, sasa hivi mwezi Januari tunaanza progamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kwa hiyo, katika mpango huu nimhakikishie Mheshimiwa Saddiq kwamba fedha itatolewa kuhakikisha miradi hii inakamilika.