Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Primary Question

MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Hivi karibuni ulifanyika Mkutano wa Dunia wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Mazingira (COP21) ambapo Katibu Mkuu wa UN alisema Mkataba uliofikiwa ni momental triumph for people and our planet aimed at ending poverty, strengthening peace and ensuring life of dignity and opportunity to all:- (a) Je, Serikali ya Tanzania ilishiriki vipi katika Mkutano huo? (b) Je, Serikali itatekelezaje maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji? (c)Je, Serikali ina mikakati gani ya kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa kila mtu?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY SALEH ALLY: Haya ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza ni suala lile la kwamba masuala ya gesijoto na tabianchi yanasimamiwa na Mkataba wa Kimataifa unaoitwa United Nation FrameWork Convetion on Climate Change. Katika mfumo wake kunakuwa na mtu au sehemu inaitwa focal point ambapo ndipo mambo yote yanapopitia.
Ni kwa nini hakuna sauti ya Zanzibar katika hiyo focal point ya Tanzania, hakuna mwakilishi wa Zanzibar ama alternatively au kutoka Zanzibar ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanalindwa katika suala hilo? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na taarifa na hali ndiyo ilivyo kwamba Zanzibar kama visiwa vingine vidogo vingi vinaweza kukabiliwa na tatizo hili la ongezeko la gesi na mabadiliko ya tabianchi na kwa hivyo hata uwepo wake upo hatarini. Je, Serikali ina mpango gani wa kudumu na wa muda mrefu katika kuhakikisha kwamba Zanzibar inatoka katika loop kubwa zaidi ya kuilinda ili iendelee kuwepo katika uso wa dunia. Ahsante.

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza anasema kwamba ushirikishwaji wa Zanzibar hasa katika suala zima la climate change pamoja na ongezeko la gesijoto kwamba Zanzibar inashirikishwa namna gani. Tumekuwa tukishirikiana na Zanzibar kwa karibu na ndiyo maana hili suala la mazingira limewekwa Ofisi ya Makamu wa Rais ili kuweza kufanya ushirikiano mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkutano wa Paris tunaouzungumza ulihudhuriwa na watu kumi na saba, watano walitoka Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kitengo cha Mazingira, ambapo tumekuwa tukishirikana kwa kila hali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi juzi hapa kuna suala lilitokea la kudidimia kwa ardhi, kuna sehemu kumedidimia kule Zanzibar, Ofisi yangu hapa ya Mazingira pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Kitengo cha Mazingira wameshiriki kufanya utafiti kuona tatizo hili linasababishwa na nini. Kwa hiyo, kwa ujumla tumekuwa tukishirikiana vizuri sana na Zanzibar hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo limezungumzwa hapa na Mheshimiwa la kuhusu Zanzibar kama kisiwa, kama tunavyojua ni kweli kabisa kwamba, sasa hivi ni dunia nzima ipo kwenye hali ngumu ya mabadiliko ya tabia ya nchi. Joto la dunia limeongezeka kutoka kwenye standard ya kawaida na kufikia nyuzi joto zero point nane tano. Dunia nzima tunahangaika sasa hivi kuhakiksha kwamba hizi nyuzi joto haziongezeki kufikia kuzidi nyuzi joto moja point tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimita kumi na tisa. Kwa hiyo, hili ni tishio kubwa ambalo lazima tuchukue hatua za dhati za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na matatizo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Mpango wa Maendeleo (framework) ambayo tumeanza nayo sasa hivi, Kitaifa tunajipanga kuhakikisha kwamba Tanzania kama Tanzania inatenga fedha za kutosha kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabianchi. Vilevile wahisani wetu, tunaendelea kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata fedha za kutosha kuhusu suala zima la mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchini Ufaransa kwenye Mkutano wa Paris, Tanzania imepata fedha dola laki tatu kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi. Vile vile tumepata fedha dola laki nne kwa ajili ya kuripoti mpango wa ripoti ya tatu kwa ajili ya kukabiliana na matatizo ya tabianchi. Pia tumepata fedha dola za marekani mia tatu hamsini na mbili, kwa ajili ya kuandaa tathmini ya kwanza ya kupunguza gesijoto nchini. Kwa hiyo, mikakati hii yote tunayoifanya na hatua ambazo tunazozifanya kupitia mpango wa maendeleo na bajeti yetu, zote hizi zitalenga katika kupunguza athari ya mabadiliko ya tabianchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niongeze machache katika kuyakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mkutano wa Paris, kila nchi ilitakiwa kutengeneza program inaitwa intended national determined contributions, yaani kila nchi itengeneze mpango wa namna ya kutekeleza makubaliano ya Paris. Katika kutengeneza mpango ule tumeshirikana na wenzetu wa Zanzibar kwa kutambua changamoto mahususi ya kwamba Zanzibar ni kisiwa, uchumi wake unategemea utalii, utalii unategemea fukwe na fukwe zinaathiriwa sana na kupanda kwa kina cha bahari. Kwa hiyo, tumefanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inabaki kama ilivyo katika uzuri wake na ubora wake ili isiathiriwe na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu focal point tumeomba kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais ndio iwe focal point ya Taifa letu katika utekelezaji wa mkataba ule. Ile Ofisi ya focal point itajumuisha Wazanzibar, tutahakikisha hilo linatokea kwa sababu changamoto zetu hizi ni changamoto za pamoja. (Makofi)

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:- Hivi karibuni ulifanyika Mkutano wa Dunia wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Mazingira (COP21) ambapo Katibu Mkuu wa UN alisema Mkataba uliofikiwa ni momental triumph for people and our planet aimed at ending poverty, strengthening peace and ensuring life of dignity and opportunity to all:- (a) Je, Serikali ya Tanzania ilishiriki vipi katika Mkutano huo? (b) Je, Serikali itatekelezaje maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji? (c)Je, Serikali ina mikakati gani ya kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa kila mtu?

Supplementary Question 2

MHE. SUZAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni wazi kwamba Tanzania imeathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, lakini vilevile sababu kubwa pamoja na kwamba kuna sababu za nje, lakini kuna sababu za ndani ambayo kubwa ni ukataji hovyo wa miti, lakini Serikali kwa muda mrefu imekuwa na kaulimbiu ya kusema kwamba kata mti panda miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa nasikiliza au naangalia vyombo vya habari hapa Dodoma ambapo ni kati kati ya nchi na Makao Makuu, Mkuu wa Mkoa alikuwa anapanda miti na ikatolewa taarifa kwamba katika miti milioni mbili na laki tatu iliyopandwa ni miti mia tisa tu imeota, sawa na asilimia 0.039. Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba wanafuatilia ili miti inapopandwa iweze kuota ili kuondoa tatizo la mabadiliko ya tabianchi?

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ukataji miti na suala la kupanda miti isiote. Sasa hivi tunaandaa mkakati wa pamoja, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, pamoja na Maliasili na Utalii na wadau wengine kuhusu mkakati wa Taifa hili katika kuhakikisha kwamba tunapanda miti ya kutosha nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tunawashirikisha kwa karibu sana wataalam wetu wa Chuo cha SUA ili kuweza kujua ni miti gani au ya aina gani inaweza kuzalishwa katika mazingira ya mkoa gani ikastawi kwa uzuri zaidi.Katika kufanya hivyo tayari report ya kwanza tumekwishaipata na tutahakikisha kwamba tunawashauri mikoa mbalimbali namna ya upandaji miti kulingana na mazingira waliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue wito huu kuwahamasisha Watanzania wote, tumeshaagiza kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kila Wilaya kwa mwaka. Zoezi hili lifanyike na tutahakikisha kwamba wataalam wetu wanawasaidia katika kuhakikisha kwamba mbegu zinapatikana, zinazokubalika kulingana na mazingira hayo na wananchi wapande miti yenye faida na wao miti ya matunda na miti ya mbao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema pia hata suala ambalo lilizungumzwa jana na Mheshimiwa hapa kwamba, unapanda miti lakini mwisho wa siku viwanda vyetu vya juice vinakosa matunda ambayo yanastahili kwa ajili ya juice hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu tunafanya utafiti pia wa kutosha kuona kwamba, miti inayopandwa, inatuletea na inatupatia matunda ambayo yatakuwa ni chanzo cha raw material kwa ajili ya viwanda vyetu vinavyojengwa hapa nchini. (Makofi)