Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM M. NYOKA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Je, lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa kwenye majengo mengine yaliyo chakavu zaidi katika Hospitali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uchakavu wa majengo ya hospitali hiyo yanakwenda sambamba pamoja na uchakavu wa vifaa tiba, ikiwemo ultra sound, Mashine ya kufulia na vifaa vingine. Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua vifaa hivyo katika hospitali hiyo? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilikuwa naongea na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ananiambia alimtembelea juzi kabla ya kuja Bungeni. Kama alivyotembea amejionea yeye mwenyewe kwanza jengo ambalo limejengwa hilo la magonjwa ya dharura, lakini alijionea ukarabati mzuri uliofanyika kwa mapato ya ndani kwenye magonjwa yanayoambukiza ambayo sasa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua wamelazwa mle ndani na Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo mengine kwa mtindo ambao sasa jengo ambalo linamalizika mwezi Oktoba umefanyika.

Mheshimiwa Spika, pia akumbuke kwamba pamoja na hilo kwa juhudi za Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mheshimiwa Jenista Mhagama, walianzisha mchakato wa kupata hospitali mpya kabisa ya mkoa, ambapo kule Mwenge - Mshindo wameweza kupata heka 276 kwa ajili ya kujenga hospitali mpya ya mkoa. Waziri wa Afya alituma watu wa kwenda kuangalia eneo, lakini ikaonekana kuna watu sita walitakiwa kufidiwa na ikafanyika tathmini ikaonekana inatakiwa milioni 700 kwa ajili ya kufidia. Sasa Waziri wa Afya ameagiza hebu tuhakiki hiyo milioni 700 kwa watu sita kwa nyumba za udongo ni nini. Kwa hiyo, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuangalia tujihakikishie hilo ili sasa tuanze michakato ya kupata Hospitali mpya kabisa ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu vifaa tiba; Mheshimiwa Mbunge atakumbuka, Bunge lililopita alikuja akilalamika kuhusu x-ray yao iliyoharibika ambayo ilikuwa ina shida ya battery na ilikuwa imeagizwa nje na imeshafika sasa na x-ray inafanya kazi. Tunampongeza sana Mbunge kwa juhudi zake hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshapeleka milioni 348 MSD, zipo cash pale ambazo ni fedha, tukimaliza hapa tukutane mimi na Mheshimiwa Mbunge ili tuwasiliane na Uongozi wa Hospitali na Mkoa ili tuweze kupanga kulingana na mahitaji anayoyasema…

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, lakini Rais wetu amepeleka direct kwenye akaunti yao milioni 110, nayo hiyo haijapangiwa chochote, kwa hiyo tunaweza vilevile kupanga kuelekeza kwenye maeneo anayoyasema.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru ahsante.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, pia kuna milioni 130 kwa ajili ya Kiwanda cha Majitiba, kwa hiyo kazi inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mungu akubariki.