Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa hati kwa Wananchi wa Meko na Basihaya baada ya maeneo hayo kupimwa?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ifahamike kwamba kuhusu upimaji wa ardhi ndani ya nchi yetu mlolongo huu umekuwa na kigugumizi kikubwa na kupelekea Serikali kupoteza mapato, migogoro ya ardhi isiyokuwa na lazima na tatu wananchi kukosa dhamana ya kwenda kuchukua mikopo maana yake wananchi kupata umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la kwanza; Ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa kwa sababu Waziri alisimama kwenye vyombo vya habari akajinasibu akasema ndani ya mwezi mmoja mtu akishapimiwa atapata hati. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi wa Basihaya wako tayari baada ya kukaa na Mwekezaji, Serikali na wananchi wa Basihaya wako tayari kulipa premium, kiwango ambacho kilikuwa ni makubaliano kati yao na premium ni kati ya 1% mpaka 1.5%. Ni lini sasa Serikali itakwenda kutoa hati katika maeneo hayo? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itapima maeneo yote ili kuweza kuondoa pengine adha ambayo watu wanaipata. Naomba niseme tu bajeti ambayo tunaendelea nayo imeainisha namna ambavyo Wizara imejipanga katika kuhakikisha kwamba maeneo yote nchini yanapimwa. Katika kufanya hilo pia tumeweza kushirikisha makampuni binafsi katika kufanya ule urasimishaji kwenye yale maeneo ambayo tayari yalikuwa yameshakaguliwa. Suala la kupima nchi nzima liko katika utaratibu wa bajeti ya Serikali na inategemea pia na upatikanaji wa fedha, lakini mpango upo ambao tutakwenda kukamilisha upimaji. Hili pia linahitaji ushirikiano na taasisi binafsi ambazo tumekuwa tukizishirikisha ambapo nyingi zimeonekana pia hazina uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo kama Wizara tunatafakari namna bora ya kuweza kukamilisha zoezi hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo amezungumzia habari ya umilikishaji katika maeneo yale, kwanza nataka tu niseme kwamba Mheshimiwa Felista anatakiwa kuishukuru sana Serikali kwa sababu maeneo yale ambayo anaombea watu kumilikishwa kisheria ilikuwa waondolewe, kwa sababu walikuwa wamevamia, lakini busara ya Wizara au ya Serikali ilipelekea kufanya mazungumzo ili wale watu waweze kumilikishwa na zoezi hilo linaendelea. Katika urasimishaji ile premium ambayo anaizungumza ni asilimia moja ambayo ni ya chini kabisa ukilinganisha na maeneo mengine ambayo wanalipa almost 2.5% na kabla ya hapo ilikuwa 15%, ikashuka ikawa 7.5%, ikaja 2.5% kwenye urasimishaji ni 1%. Kwa hiyo wanachajiwa kiasi cha chini kabisa kuweza kuwawezesha kupata umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la Hati, nadhani ninyi wenyewe ni mashahidi, Mheshimiwa Waziri pia ameweza kukaa ofisini na kuweza kuwapigia watu mmoja mmoja kuja kuchukua hati zao. Nimezunguka almost nchi nzima nikienda kugawa hati katika maeneo mbalimbali. Kuna hati ziko tayari lakini Watanzania hawaji kuchukua hati zao, lakini ukija nje wanasema hati hazitoki. Kasi ya utoaji hati kama tulivyosema ni ile ile ndani ya mwezi mmoja kama halmashauri imekamilisha taarifa zote, hati yako unaipata na zoezi hilo linafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania wale wote wanaohitaji kupata umiliki wa ardhi kama ambavyo ameongelea Mheshimiwa basi wawe tayari, pia ukishapeleka maombi yako uhakikishe umekwenda mpaka mwisho na umechukua hati yako. Wizara ndiyo custodian wa hati.

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU Aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa hati kwa Wananchi wa Meko na Basihaya baada ya maeneo hayo kupimwa?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa nilipofika ofisini kwa Mheshimiwa Waziri akaniambia kwamba Meko tayari amepima viwanja 840 na akanijulisha kwamba amepima viwanja 4,000 Basihaya. Sasa kwa kuwa Chasimba, Chachui Chatembo na Kasangwe Burumawe, Kissanga na maeneo mengine ni maeneo ya Jimbo la Kawe na yaligubikwa na migogoro ya ardhi, sasa ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakwenda pamoja nami, Mbunge wa Kawe ili tukamalize migogoro iliyodumu kwa muda mrefu? (Kicheko)

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amempa Mheshimiwa Njau. Pili nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima, mimi Askofu Gwajima nilikuwa simjui lakini amenitafuta kwa shughuli hizi za kero za wananchi wa Kawe hata kabla hajawa Mbunge, ilinilazimu kutoka kwenye kampeni, kuacha kampeni zangu Isimani kwenda kumsikiliza Dar es Salaam kwa sababu ya hiki. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima….

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mimi najua angeuliza Mheshimiwa Halima ningemjibu, ninyi siwajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima tukimaliza Bunge hili, nimepanga ratiba ya kwenda kukamilisha kero za migogoro ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatatua tatizo la Chasimba, Chatembo, Chachui kwa sababu mimi nilifanya kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwaonea huruma wale wananchi waliokuwa wafukuzwe. Kwa hiyo tutakwenda pamoja tutakwenda Basihaya, tutakwenda Chasimba na wananchi wanaoishi huko wajue kwamba nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kuhakikisha kwamba jambo hili la kero za wananchi kule sasa linaisha. (Makofi)