Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:- Kituo cha Polisi Nkome kina Askari wa kiume pekee hivyo hata huduma kwa akina Mama ikiwemo upekuzi hufanywa na Askari wa kiume:- Je, ni lini sasa Serikali itapeleka askari wa kike katika kituo hicho?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nisikitike sana kwa majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri hayaendani kabisa na maeneo ya Jimbo langu la Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri Waziri mhusika Mheshimiwa Kangi Lugola familia yake maana yake Mama yake na Dada zake wanaishi kwenye Jimbo langu, na Mheshimiwa Kangi Lugola mwenyewe ameishi kwenye Jimbo langu anayajua mazingira na majibu yaliyotolewa siyo sahihi. Kwa mfano, ukichukulia kituo cha Nyarugusu, Nyakagwe, Buziku, Bwanga na Chato Vijijini haya yote ni mazingira ambayo karibia tunafanana lakini wenzetu tayari wana Askari wa Kike. Sasa ninataka kujua ni lini Serikali itanipatia Askari wa Kike kwa kuwa majibu waliyotoa ni ya uwongo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Centre ya Nkome ni centre ya tatu kwenye Mkoa wetu wa Geita kwa ukubwa. Kituo kilichopo pale kinaongozwa na Inspekta na nimekijenga mimi kama Mbunge. Tatizo linaloonekana hapa kwamba hakuna makazi ya kuweza kumuweka Askari wa Kike, wajibu wa kujenga makazi bora ya askari ni ya Wizara.

Je, ni lini Serikali itachukua dharura ya kwenda kujenga hiyo nyumba anayotakiwa kukaa Askari wa Kike? (Makofi)

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba taratibu hasa zinazohusu upekuzi ni lazima Askari wa Kike ampekue mtuhumiwa wa kike. Majibu mazuri kwenye swali la msingi ameyasema Naibu Waziri wangu, kwamba hata pale ambapo kunakuwa na changamoto ya kutokuwepo Askari wa Kike upo utaratibu ama wa kumtumia mgambo wa kike ama kumtumia Mke wa Askari ambaye yuko jirani na mahali ambapo kuna mtuhumiwa. Najua suala la Mheshimiwa Musukuma nimeshamwagiza tayari Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita kupeleka Askari wa Kike kwenye Kituo cha Polisi cha Nkome. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamekuwa wakiomba tuwapelekee Askari wa Kike kwenye vituo vya Polisi. Ninajua Waheshimiwa Wabunge Askari wa Kike wanapokuwa katika maeneo mbalimbali ni faraja kwa wananchi kwa sababu Askari wa Kike wao wanaruhusiwa hata kuwapekua watuhumiwa wa kiume. Kwa hiyo ninajua kwamba Mheshimiwa Musukuma anatarajia kuona Askari wa Kike katika maeneo mbalimbali ya vituo vya Polisi. Kwa hiyo nimpe faraja kwamba pale ambapo kuna changamoto kama hiyo na juzi tumepata Askari kutoka Chuo chetu cha Polisi Moshi, tutawapelekea Askari wa Kike.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi/ Kicheko)