Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme. Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, moja ya changamoto kubwainayochelewesha kukamilika kwa wakati kwa miradi yah ii ya REA ni tofauti ya size ya transfoma iliyopo kwenye mikataba ya kVA 33 na ukubwa na laini ambazo wanachukulia ule umeme. Jambo hili limesababisha kuchelewa kwa Miradi ya REA ya kukamika kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini, kwenye vijiji vya Kulasi na vijiji vya Mswaha Majengo, nguzo zimesimama kwa zaidi ya miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatoa maelekezo kwa REA kuharakisha utatuzi wa changamoto hizi ili wananchi hawa waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo la Korogwe Vijijini zipo kata tano ambazo vijiji vyake vyote katika kata hizo havijafikiwa na huduma ya umeme. Kata za Kizara, Foroforo, Kararani, Mpale na ya Mswaha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kuwahakikishia wananchi wa kata hizi kuiwapa kipaumbele na kupata umeme kwenye mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mnzava, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mnzava, pampja na kwamba si Mbunge wa muda mrefu, lakini kafanya mambo makubwa sana kwenye jimbo lake hata nilizotembelea. Baada ya kusema hayo basi napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kweli, katika Kijiji cha Kurasi Kibaoni pamoja na Mswaha Majengo, kuna transfoma zilifungwa za kVA 33, lakini tumeshamwelekeza mkandarasi kuanza kushusha kutoka kVA 33, kwenda kVA 11 kuanzia Jumamosi iliyopita. Kwa hiyo, vijiji viwili vya Kulasi pamoja na Mswaha vimeshaanza kupelekewa umeme na vitapata umeme mwisho wa wiki hii. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mnzava katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kweli zipo kata tano ambazo zilikuwa hazijapata umeme katika Jimbo la Korogwe Vijijini na kati ya kata tano tayari kata moja ya Mswaha- Majengo imeshaanza kupelekewa umeme. Zimebaki kata nne ya Foroforo pamoja na Kirarani ambazo nazo zinaanza kupelekewa umeme kuanzia Julai mwaka huu na kufikia Juni, mwakani nafikiri zitakuwa zimepatiwa umeme. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mzava, aendelee kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nilipotembelea tarehe 22 kwa Mheshimiwa Mnzava, Kijiji cha Mkalekwa pamoja na Welei vilipelekewa umeme na nikaagiza Kijiji cha Kulasi nacho kiwashwe umeme. Kimeshawashwa umeme tangu tarehe 28 mwezi uliopita. Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Mnzava tuendelee kushirikiana. Ahsante sana.

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme. Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Serikali ilitoa maelekezo kwamba kwamba wananchi vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 bila kujali kama ni kupita REA au TANESCO, lakini agizo hili bado halitekelezwi na wananchi maeneo mengi wanapata shida kwa kutakiwa kulipa gharama ileile ya zamani. (Makofi)

Je, nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili? Nashukuru.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa
Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuanzia tarehe moja Mei mwaka huu tumetoa maelekezo nchi nzima kwamba pamoja na kwamba katika baadhi ya maeneo ambako REA ilikuwa haijafika, kuunganishwa umeme ilikuwa ni tofauti na 27,000; lakini ili tuweze kushambulia, vijiji vyote vipelekewe umeme haraka iwezekavyo Serikali imetoa maelekezo kwamba vijijini umeme wataunganishiwa kwa 27,000 na si vinginevyo, iwe anapeleka TANESCO, iwe anapeleka REA, iwe anapeleka mkandarasi yeyote aliyepewa kazi na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kote, hakuna mahala ambapo umeme utapelekwa tofauti na 27,000 ili mradi ni vijijini. Kwa hiyo, maagizo haya nimeyatoa na Serikali imeyatoa na tutaendelea kufuatilia hilo. Tupe ushirikiano Mheshimiwa Mbunge ikibidi tutatembelea jimbo lako ili tuwafafanulie vizuri wananchi. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. (Makofi)

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme. Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?

Supplementary Question 3

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Waziri, utakumbuka siku za karibuni umefanya ziara kwenye Mkoa wa Mtwara na hasa Wilaya ya Masasi ili kuweza kuona athari zilizopo hasa zaidi kwenye vijiji vile ambavyo vinapitiwa na umeme mkubwa ukielekea Wilayani Masasi.

Sasa swali, toka umeondoka takribani ni wiki mbili sasa, unaweza kutueleza ni hatua gani na ni kazi gani inatakiwa kufanyika katika maeneo hayo?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kuwa ziko hatua tatu, la kwanza katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ingawaje nilifika jimboni uliniagiza tu haukuweza kuwepo, lakini tumekuwashia vijiji viwili.

Kwa hiyo, ni hatua ya kwanza imefanyika, lakini hatua ya pili tumeainisha maeneo yote ya Jimbo la Masasi ambapo umeme haukufika, wakandarasi wameshapewa maeneo hayo na mengine tumewapa TANESCO kwa sababu bei ni moja ili maeneo hayo yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya tatu mkandarasi ameshapeleka nguzo na vitendea kazi maeneo yote ili kazi iweze kwenda kwa haraka zaidi. Hizo ndizo hatua tumechukua. (Makofi)

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme. Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?

Supplementary Question 4

MHE. ANNE K. MALECELA:Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Jimbo la Mheshimiwa Mnzava ni mpakani na kijiji changu cha Kongei ambako nimezaliwa na umeme kwenye kijiji hiki umefika muda mrefu, lakini kuna Vitongoji vya Mabambara, Ihindi na Idurundi, huenda vimesahauriwa kabisa. Mheshimiwa Waziri unaniambia nini katika hili?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda nijibu swali moja la Mheshimiwa Mama yangu Anne Kilango Malecela na nimshukuru sana kwa kazi nzuri ya kufuatilia sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya nishati na kwa kuwa swali lake la nyongeza ameulizia katika usambazaji wa umeme kwenye vitongoji vilivyosalia katika Kijiji chake cha Kongei.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu kwamba Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa tisa ambayo mradi wa ujazilizi awamu ya pili ambao upo hatua za kumpata mzabuni, Mkoa huu wa Kilimanjaro umo kwenye mikoa hiyo tisa na nimwagize Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro na wa Wilaya ya Same azingatie vile vijiji ambavyo vimepatiwa umeme kikiwemo Kongei, lakini vipo vitongoji ambavyo havina umeme ili waendelee kusambaza kupitia umeme wa ujazilizi awamu ya pili ambapo Bunge letu mmetupitishia takribani shilingi bilioni 169 na tunawashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:- Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme. Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?

Supplementary Question 5

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, katika Wilaya ya Chunya, Kijiji cha Itumbi, ni sehemu ambayo Wizara ya Madini imetenga vitalu vya wachimbaji wadogo wadogo kwa Wilaya nzima na Wizara ya Madini ni sehemu ambapo inajenga kituo cha ushauri kikubwa kwa wachimbaji wadogo wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza, kijiji hiki hakijapitiwa. Je, Serikali inatoa tamko gani kwenye kijiji hiki cha muhimu sana?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambalaswa katika swali lake la nyongeza.

Kwanza ningependa sana nimshukuru katika mambo mawili, la kwanza, alituletea maeneo yote ambako kuna uchimbaji wa madini, na sisi kutpitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) tumeshaainisha Kijiji cha Itumbi kwa sababu ni kijiji cha mfano kwa wachimbaji wadogo na tumeshatenga transfoma mbili za kVA 315 kila kijiji, kikiwemo Kijiji cha Itumbi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kijiji cha Itumbi kitapelekewa umeme kwa sababu tunajua umuhimu wa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mpango huu tumeuanza kwa nchi nzima, tumemaliza kufunga transfoma tatu katika Mgodi wa Nyakafuru, tumewasha mwezi uliopita na sasa hivi tunahangaika na kuwasha kwa wachimbaji wadogo eneo la Kidirifu na Itumbi, pamoja na K9 kule Geita, pamoja na Kidirifu na Society kule Katavi. Kwa hiyo, ni wananchi wote ambako kuna migodi, shuguli za uchimbaji tunazithamini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita nilikwenda Mwakitoryo, Mwakitoryo nao watafungiwa transifoma ya kVA 315 Ijumaa wiki hii. Kwa hiyo, maeneo yote ya migodi likiwemo eneo la Itumbi, Mheshimiwa Mbunge yatafungiwa umeme natutakuja kuwasha umeme wenyewe hapo Itumbi kwa wachimbaji wadogo. (Makofi)