Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Christopher Kajoro Chizza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:- Wafanyabiashara wa Wilaya ya Kakonko wanapenda kujisajili BRELA ili kurahisisha biashara zao na kulipa kodi stahiki lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa kukosa Vitambulisho vya Taifa (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha zoezi la kutoa Vitambulisho vya Taifa ili wananchi waweze kuvitumia katika shughuli za maendeleo? (b) Kuna wananchi wanaokaa katika mipaka kati ya Tanzania na nchi nyingine; je, Serikali imewawekea utaratibu gani wa kuwapa vitambulisho wananchi hao kwa haraka bila kuathiri malengo ya zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vitambulisho hivi vya Taifa ni muhimu kwa maendeleo na vinatambuliwa, hata mtu akiwa nje ya nchi vitambulisho hivi vinatabuliwa. Sasa kwa sababu vitambulisho hivi ni muhimu lakini ukitazama zoezi linaloendelea linasuasua na hususan kwa wananchi wa kawaida, maana watu ambao wamevipata ni watu kama sisi Wabunge na watumishi wa Serikali, wananchi wa kawaida kwa kweli hawajavipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali inaendelea kukamilisha usajili wa watu wenye sifa kwa kuchukua alama za vidole, picha na saini za kielektroniki. Kwa kuwa katika Wilaya ya Kakonko takribani kata tano kati ya 13 wamekwishakamilisha zoezi hili, kwa nini sasa vitambulisho hivi hawavipati? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninapenda kujua sasa, mara ya mwisho Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema Watanzania takribani milioni 16 wamekwishapata vitambulisho, je, hivi sasa ni wananchi wangapi wa Tanzania wakiwemo wale wa vijijini, wote kwa ujumla wamekwishapata vitambulisho hivi muhimu? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chiza, ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa wakiuliza maswali yao kwa umakini wa hali ya juu. Lakini kuhusiana na hoja zake mbili kwa pamoja, nataka nimjibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Nabu Spika, moja, nina mashaka juu ya takwimu ambazo amezitoa akimkariri Mheshimiwa Waziri kwa sababu uhalisia uliopo ni kwamba mpaka sasa hivi tumeshatoa vitambulisho takribani milioni tano huku vitambulisho takribani milioni 13 vikiwa vipo katika hatua za mwisho kutolewa, wakati malengo yetu mpaka itakapofika mwezi Desemba ni kama milioni 24.2. Kwa hiyo utaona kwamba tupo vizuri kwa sababu milioni 18 ni kama vile tayari process yake imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikijibu swali lake la mwanzo sasa kwamba inawezekana miongoni mwa watu ambao wananchi wake wa Kakonko ambao hawakupata vitambulisho ni hawa ambao vitambulisho vyao ni hivi milioni 13 ambavyo vinafanyiwa kazi. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, muda si mrefu vitambulisho hivi vitatolewa na wananchi wake wengi nina uhakika watakuwa wamepata vitambulisho hivyo kama watakuwa wamekamilisha, kama nilivyosema, processes zote za kuweza kujisajili.