Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Primary Question

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:- Wananchi wengi katika Kata za Fukayosi na Kiwangwa Bagamoyo wanalima mananasi kwa wingi sana. Je, nini mkakati wa Serikali kuhusu kuwajengea viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuboresha kipato cha wakulima hao?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu haya mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nichukue nafasi hii kuwapa pongezi wawekezaji wa ndani, wazawa kwa kujenga viwanda hivi ambavyo vimepunguza tatizo la soko. Lakini pamoja na uwepo wa viwadna hivi viwili tatizo la soko bado ni kubwa sana na msimu uliopita mananasi yaliozea shambani na tatizo linaongezeka kwa utaratibu uliopo sasa hivi wa ununuzi wa mananasi haya ambao utaratibu huu unahushisha madalali kusababisha usumbufu mkubwa na wakati mwingine kupoteza mapato kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari kuwahamasisha wawekezaji hawa ili waweke utaratibu rafiki utakaowawezesha wakulima kuuza zao lao la nanasi kwa urahisi zaidi na kwa kuwapatia kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile zao hili ni zao la kibiashara na linafanya vizuri, linaipatia kipato Serikali pamoja na wakulima, sasa swali langu, je, Serikali iko tayari..., samahani pamoja na kufanya hivyo vizuri mkulima inabidi apambane yeye mwenyewe kwa hatua zote kuanzia kuandaa shamba, kupanda, kupalilia mpaka kuvuna na kadhalika na kubeba gharama zote.

Je, kwa kutambua umuhimu wa zao hili Serikali iko tayari sasa kuwaunga mkono wakulima hawa kwa kuwapa ruzuku katika pembejeo kama vile mbolea na pembeje zingine? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA):
Mheshimiwa Naibu Spika,ni dhamira ya Serikali kuhakikisha wakulima wa mananasi wa Bagamoyo wananufaika na kupata tija kupitia kilimo cha mananasi. Kumekuwepo na utaratibu wa katikati hapo kuingiza watu wa kati ambao mwisho wa siku wanawafanya wakulima hawa wasiweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tutaendelea kuweka mipango madhubuti na miundombinu rafiki ili kumfanya mkulima huyu wa nana wa Bagamoyo apate soko la uhakika moja moja kupitia kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi yangu niliwahi kuzungumza naye pale Bagamoyo katika Kijiji cha Dutumi, Kata ya Dutumi tumeshazungumza tayari na muwekezaji Sayona Fruits Company Limited ambao wako tayari kushirikiana na Serikali na tumeanza kuwaandaa vijana na tayari ekari 50 imeshatengwa na tutachimba visima viwili na watu wa SUA wameshakwenda pale Dutumi, wameipima ardhi, wamejua mwekezaji anataka nini, baadae tutaanza utaratibu mzuri sasa kuhakikisha kwamba ile mbegu itakayokwenda kupandwa pale kwa matunda ambayo mwekezaji anahitaji atanunua moja kwa moja kutoka kwa wakulima Kijiji cha Dutumi na hivyo itakuwa soko kuwa la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili amezungumza kuhusu ruzuku na kuwawezesha wakulima. Niseme tu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu pia mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika hatua hii ya awali ningeshauri kwanza wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo kuitumia benki yetu ya kilimo ambayo pia ina fursa ya kuwawezesha kupata mikopo ambayo itaongeza tija katika uzalishaji wao ili baadae basi wasipate shida katika uzalishaji wao. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi nipende tu kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Mavunde Naibu Waziri. Lakini kwanza nipende kusema kwamba tumemsikia Mheshimiwa Kawambwa lakini pia na Wabunge wote ambao wamekuwa wakizalisha mazao ya matunda pamoja na mboga mboga, na nipende tu kusema kwamba kwa sasa tumeandaa kongamano maalum la uwekezaji katika nyanda za juu Kusini ambao tutalifanya Mbeya Jumatatu na Jumanne. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge Kawambwa tutafanya hivyo pia katika Mkoa wa Pwani tukitambua kwamba na wenyewe wana kilimo cha matunda na mboga mboga na tutaenda pia katika kanda zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili tunakusudia pia kuandaa kongamano maalum la kuvutia uwekezaji katika kilimo, mifugo na uvuvi na tutashirikiana na Benki ya Kilimo pamoja na Wizara husika, kwa hiyo tuombe tu Wabunge tushirikiane endapo kuna mahitaji mahusui basi tuweze kupata ili tuweze kushirikiana katika kuvutia uwekezaji huu, nakushukuru. (Makofi)