Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:- (a) Je, ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B wamepata nafasi ya kujiunga na Jeshi kuanzia mwaka 2015? (b) Je, mgawanyo wa idadi ya vijana wanaojiunga na Jeshi kwa kila wilaya nchini upoje?

Supplementary Question 1

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake japo hayajaniridhisha kwa sababu swali langu la msingi nilihitaji kujua ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wamepata ajira katika jeshi kwa miaka mitatu, lakini amenipa jibu la jumla la Zanzibar yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka kujua ni lini vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watapata ajira katika jeshi ili kuondoa malalamiko yaliyopo hivi sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa manug’uniko ni mengi yanayotokana na vijana kujitolea kwa muda mrefu lakini hawapati ajira. Ni mkakati gani ambao Serikali umeupanga ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira hiyo kwa kuzingatia pia jinsia maana hapa katika orodha yake inaonyesha wanaume 720 wanawake 280?

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza anasema sikumpa takwimu za ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na B waliojiunga na JKT. Katika jibu langu la msingi nilitoa takwimu za jumla za vijana wanaochukuliwa kutoka Zanzibar na nikaeleza kwamba jukumu la kupanga idadi kwa Wilaya za Zanzibar linafanywa na SMZ. Kwa hivyo takwimu sina na Mheshimiwa akizihitaji itabidi azipate kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu wao ndiyo wanapanga kwa mujibu wanavyoamua, sisi tunakabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wao wanagawa wanavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika hilo hilo la kwanza alikuwa anauliza lini vijana watapata ajira ili kuondoa malalamiko. Nataka ieleweke kwamba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa lazima vijana waelewe kwamba siyo ajira, kujiunga na JKT ni kwenda kupata mafunzo ya kijeshi pamoja na study za kazi. Wachache watapata ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, walio wengi watabidi wajiajiri wenyewe au waajiriwe na sekta binafsi. Hili ni muhimu lieleweke, wasielewe kwamba kujiunga na JKT ndiyo ajira. Tunachukua vijana wengi na nilitoa takwimu hapa wakati wa bajeti yangu kwamba tunachukua takribani vijana 20,000 kwa mwaka. Vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa ku-observe kuchukua wote hao katika ajira, watapata wachache na walio wengi watakuwa wamepata study za kazi ili waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni mkakati gani wa kupatia ajira na kwa kuzingatia jinsia, hawa tuliowataja ni vijana wanaojiunga na JKT na siyo ajira. Kwa maana hiyo kule wanapofanya usaili kuna vigezo ambavyo vinafuatwa, mara nyingi wasichana hawajitokezi kwa wingi lakini wanaojitokeza wengine wanakosa sifa zinazotakiwa na ndiyo maana unaona kuna tofauti ya idadi hapa. Kwa hiyo, mkakati uliopo ni kuwasaidia vijana hawa, wale wanaokosa ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kuwapa study za kazi ili waweze kuajiriwa na sekta nyingine pamoja na kujiajiri wao wenyewe.