Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Primary Question

MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:- Serikali iliingia Mikataba na Uwekezaji na Wadau mbalimbali kwenye Sekta tofauti ambayo kwa sababu mbalimbali imesitishwa na Serikali? (a) Je, ni Mikataba mingapi imesitishwa na ni sekta zipi zinaongoza? (b) Je, Serikali imeingia gharama kiasi gani, katika kesi zilizofunguliwa Mahakamani na kusitishwa kwa Mikataba hiyo? (c) Je, Serikali imepata faida au hasara gani kwa kusitisha Mikataba hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaliyojibiwa kwa ufanisi, na weledi wa hali ya juu, pamoja na hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza na kabla sijauliza maswali hayo nataka nipongeze sana Serikali kwa hatua iliyochukua kwa kusitisha mikataba yote ambayo ilikuwa inaonekana wazi haizingatii maslahi mapana ya wananchi wa Tanzania. Vilevile niipongeze Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali alizoziainisha Mheshimiwa Waziri za kuhakikisha kuwa sasa mikataba itakuwa inafatiliwa kwa ukaribu zaidi. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kutokana na mwenendo mzima na utaratibu wa malalamiko mengi yanayojitokeza katika sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji na katika sekta nyingine muhimu za kiuchumi ni dhahiri mikataba mingi iliyoingiwa imekuwa haiwanufaishi wadau wa sekta hizi hasa wakulima, wafugaji na wavuvi. Ningependa sasa Serikali ituambie wana mkakati gani maalum wa kuhakikisha kuwa mikataba inayoingiwa na wawekezaji wa kilimo, ufugaji, uvuvi, uletwaji wa pembejeo mbalimbali, masoko n.k sasa hivi yanapitiwa upya na kuhakikisha kuwa yanazingatia maslahi mapana ya sekta hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mkoa wangu wa Songwe na hususani Wilaya ya Ileje ina migodi ya makaa ya mawe, wa Kiwira pamoja na ule Mlima Kabulo na kwa muda mrefu sasa mgodi ule haufanyi kazi kwa sababu mkataba wake ulisitishwa na mgodi ule ulikuwa unaajiri takribani watu 7000 na zaidi. Je, ni lini sasa mkataba ule utapitiwa upya ili ule mgodi uanze kufanya kazi? Naomba sana Serikali izingatie hilo kwa sababu tayari tunaathirika kiuchumi.

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kila wizara na kila sekta inapeleka rasimu za mikataba ambayo wangependa waingie na wadau wao hapa nchini au nje ya nchi kwa Mwanasheria Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza hapo mwanzoni mikataba mingine ni mizuri, mingine ina mapungufu, mingine ni mibaya ile ambayo ni mizuri kila wizara ambayo tayari imeshatoa taarifa yake hapa wametueleza mafanikio yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tu Wizara ya Madini imetueleza jinsi faida inavyopatikana kutoka sekta ya madini, kutokana na mikataba ya uuzaji madini yetu ulimwenguni. Na mashirika yote yaliyo chini ya Wizara ya Madini ikiwa ni pamoja na STAMICO wamekuwa wakirejesha Serikalini pato kubwa ambayo hiyo ni sehemu ya faida hiyo. Ni lazima tuangalie kwa makini mikataba mingi ina udanganyifu na tunaposaini mikataba hii tunaweza kudanganywa na ndio maana wizara yangu imeona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho na kusahihisha mapungufu yote ya wizara zote na taasisi zote zoezi hilo linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na madhumuni ya kumuweka wakili wa Serikali kumsaidia Mwanasheria Mkuu ni hilo kuangalia ubora wa mikataba yote ambayo Serikali na Wizara zake na taasisi zote inaingia na zoezi hilo linaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mgodi wa Kiwira ninaamini kwamba Mheshimiwa Mbunge jana ulisikiliza hotuba ya Waziri wa Madini alivyosifia ule mgodi mpya wa Kibulo ambao ulianzishwa mwezi Novemba, 2018 na ilipofika Machi, 2019 umeshatoa faida ya milioni 12.9 na kuilipa Serikali milioni 4.7 ni malipo mengine yanayofikia milioni 2.7. pia mgodi ule tayari umeshaleta kinu ambacho kinachakata mkaa unaouzwa katika nchi zifuatazo, Kenya Uganda, Rwanda, Burundi na China.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna sehemu ambazo lazima tuangalie mkataba huu ili tuweke maboresho hasa katika ajira lakini kipimo cha mikataba isiwe tu udhaifu wake lazima tutazame pia faida zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali kama haya tuanze kuyauliza je faida ni zipi na hasara ni zipi. Na nadhani katika mgodi wa Kiwira na migodi mingine ya makaa ya mawe tutaendelea kupata nishati mpya kabisa na imetathminiwa kimataifa kwamba mkaa unaotoka Tanzania na hasa unaotoka kule Liganga ni kati ya mikaa bora duniani ambayo haitosi gasi chafu kama mikaa mingine duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa kwamba tutatazama masuala ya ajira lakini nina hakika kutokana na faida kubwa tunayopata na mgodi wa Kiwira kama Waziri Biteko alivyotueleza jana tupo katika mwelekeo mzuri, ahsante. (Makofi)