Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- (a) Je, Viwanda vilivyopo nchini vina uwezo wa kubangua korosho kiasi gani? (b) Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza ubanguaji wa korosho?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia hiyo takwimu utajua wazi kwamba bado kiwango chetu cha ubanguaji ni kidogo kwa sababu msimu wa 2017/2018 Tanzania tulifikisha mavuno ya korosho Tani 312,000, kwa hiyo kinachobanguliwa ni kiasi kidogo sana. Sasa kwa kuwa Mkoa wa Mtwara na Lindi wameshatenga maeneo ya uwekezaji hususani viwanda vya korosho, je, Serikali itatoa vivutio maalum ikiwemo kufuta baadhi ya kodi ili wawekezaji hawa waje Mikoa ya Mtwara na Lindi kuwekeza Viwanda hivyo vya Korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mavuno ya korosho hutegemea sana upatikanaji wa pembejeo na niipongeze Bodi ya Korosho kwa sababu wale wakulima ambao hawajalipa fedha zao za korosho inatoa mkopo, lakini kuna urasimu mkubwa sana wa kupata hiyo pembejeo. Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa badala ya mkulima kuzaminiwa na AMCOS na Serikali ya Kijiji na Mkurugenzi waondoe huo mlolongo mrefu ili wakulima wadhaminiwe na AMCOS na kupewa hiyo sulfur (Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jitihada kubwa anayofanya katika kufatilia juu ya maendeleo mazuri ya zao hili la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusiana na kuweka vivutio kwa ajili ya uwekezaji kimsingi Serikali imekuwa ikifanya hivyo hasa kwa viwanda vyote ambavyo vinatumia malighafi inayozalishwa hapa nchini; na hivi karibuni tumeshuhudia kwamba kodi zimeondolewa kwa ajili ya kuwezesha viwanda hivyo viweze kufanya kazi. Hali kadhalika tunajaribu kuendelea kuona kwamba vile Viwanda ambavyo vilikuwa kwa siku za nyuma vinabangua korosho lakini kwa sasa vimekuwa havibangui na vitaendelea kuwa kama maghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunajaribu kuwaunganisha sasa na Wawekezaji wengine ili waweze kutumia viwanda hivyo katika kuwekeza mashine na waweze kubangua korosho pasipo kulazimika kuanza kujenga upya pamoja na maeneo hayo ambayo yametengwa. Niupongeze sana Mkoa wa Lindi wa Mtwara kwa jitihada ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la pili, kuhusu pembejeo suala lake alivyolizungumza nimelisikia. Niseme tu kwamba tungependa zaidi kuona kwamba pembejeo hizo kwa wale wanaoagiza na kuzileta waweze wao wenyewe kuziuza kwa kulingana na uhalisia wa maeneo kuliko tu kutegemea kwamba Serikali yenyewe iwe inaingilia halafu badala yake pengine kutokuwa na usimamizi unaotakiwa. Hata hivyo mawazo yake tunayachukua na yataendelea kufanyiwa kazi.