Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:- Wilaya ya Mbozi ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe inapakana na Wilaya ya Songwe; Wilaya hizi mbili hazijaunganishwa kwa barabara hivyo Wananchi wanaotoka Wilaya ya Songwe kwenda Makao Makuu ya Mkoa hulazimika kupitia Mkoa wa Mbeya? (a) Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara ya changarawe kutoka Kata ya Magamba ambayo ipo Wilaya ya Songwe kupitia Kata ya Magamba ambayo ipo Mbozi? (b) Kata za Magamba, Itumpi, Bara, Itaka na Halungu hazina vivuko na madaraja hali inayosababisha usumbufu kwa Wananchi; Je, ni lini Serikali itajenga vivuko katika Kata hizo?

Supplementary Question 1

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kwa kuwa barabara hii inapita eneo muhimu sana eneo ambalo wanachimba makaa ya mawe, Kijiji cha Magamba, na kwa kuzingatia pia kwamba barabara hii inaunganisha wilaya mbili kwa maana ya Wilaya Mbozi pamoja na Wilaya ya Songwe, je Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanza kufikiria kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sehemu (b) ya swali hili haikujibiwa, inayohusu vivuko pamoja na madaraja Kata za Itumpi, Halungu, Itaka pamoja na Bara, je, Serikali inawaambia nini wananchi wa maeneo haya ambao wanakosa mawasiliano ya vivuko na wanakosa maeneo ya kuvukia; je, Serikali inawaambia nini na kwa kutokujibu vizuri swali hili, je, Serikali haioni kwamba wananchi hawa wataendelea kuteseka kwa kuwa maeneo mengi hawa wananchi hata kuvuka kutoka kijiji kimoja kwenda kingine inakuwa ni shida kubwa sana? Je, Serikali haioni kuwa ni kuwatesa wananchi wa maeneo haya?.

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, Mheshimiwa Mbunge Sera ya Chama cha Mapinduzi, Sera ya Wizara ni kuunganisha mikoa kwa lami; lakini tunaendelea kuziunganisha wilaya kwa barabara za changarawe. Itakapofikia tumemaliza kwanza sera yetu ya kuunganisha mikoa kwa lami; na nishukuru kwamba Mkoa wako tayari umeshaunganishwa kwa lami tutaendelea sasa na barabara za wilaya, kwa hiyo uvute subira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madaraja na vivuko, sijui tofauti yake ni nini, lakini nafikiri umezungumzia madaraja; suala la madaraja tunaendelea kujenga kwenye barabara zote za TANROADS pamoja na barabara za TARURA pia. Kwa hiyo tutaendelea kujenga kadiri ya ukusanyaji wa fedha kutoka kwenye Mfuko wa Barabara. Nina imani na wewe mwenyewe unafahamu, TARURA sasa hivi inakwenda vizuri, matatizo yake tu ni kwamba fungu halijawa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa sababu linatokana na Mfuko wa Barabara na kuna Kamati inaendelea sasa ili iweze kuweka uwiano ambao ni mzuri kulingana na barabara za TARURA baada ya muda tutakuwa na hela ya kutosha madaraja hayo ambayo unayaita vivuko pia yatajengwa.