Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuja na majibu mazuri sana yenye faraja kwa wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa wakilazwa katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala sasa mashine za kufulia zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nampongeza sana kwa majibu hayo mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mashine za kufulia katika hospitali hizo zinakosa pia mashine nyinginezo za vipimo zikiwemo mashine za MRI, mashine za kupima ubongo na mashine nyingine hali ambayo inawalazimu wagonjwa kufuata huduma hiyo ya vipimo katika Hospitali ya Muhimbili. Wanapofika katika Hospitali ya Muhimbili, vipimo hivyo hupewa kwa gharama mara mbili ya ile bei ya kawaida ya Hospitali ya wagonjwa waliopo Muhimbili. Je, Serikali kwa nini inatoa gharama tofauti wakati hospitali hizi zote ni za Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwanza naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza Ilani yake ya Chama kwa kujenga Hospitali za Wilaya 67 na zimepewa fedha karibia bilioni 1.5 na milioni 500 wameongezewa ikiwemo Kigamboni katika Jiji la Dar es salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuhakikisha hizo hospitali 67 ambazo zitajengwa kuwa na mashine na vipimo vyote vinavyostahili katika kila hospitali.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es salaam amekuwa ni Mbunge wa mfano katika Wabunge wa Viti Maalum katika ufuatiliaji wa mambo mbalimbali yanayotokea katika Mkoa wa Dar es salaam na sisi kama mmoja wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam nampongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sasa hivi Serikali inafanya maboresho makubwa katika Sekta ya Afya na tumeona kwamba kuna uhitaji wa kuboresha na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za afya hususan vile vipimo mahsusi kama uwepo wa MRI, CT Scan na vipimo vingine mahsusi ambavyo hapo awali vilikuwa vinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivyo, kupitia mpango wetu wa sasa hivi wa kuboresha huduma na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa Serikali imedhamiria kupanua wigo kuhakikisha kwamba vipimo kama CT Scan na MRI zitaanza kupatikana katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ameuliza kwa nini baadhi ya vipimo vinachajiwa mara mbili zaidi ya zile gharama halisi ambazo zipo pale. katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tumeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba rufaa inazingatiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni Hospitali ya Taifa, maana yake ni kwamba unapokwenda pale unahakikisha kwamba umetoka katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya, Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, umekwenda Hospitali ya Kanda Mloganzila wameshindwa pale sasa unakwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na baadhi ya watu ambao katika magonjwa ya kawaida ambayo yangeweza kutibiwa katika maeneo mengine wanakwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Ili sasa kuweka mfumo wa rufaa ukae vizuri, mtu ambaye amekwenda kwa mfumo wa rufaa gharama zake zinakuwa chini, yule ambaye amekwenda kwa mfumo nje ya rufaa, yule anahesabika kwamba ni mgonjwa amekwenda kama mgonjwa binafsi na gharama zake mara nyingi zinakuwa zipo juu. Lengo ni kuhakikisha kwamba mfumo wa rufaa umezingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni nini mkakati wa Serikali kuelekea katika ujenzi huu ambao tumejenga hospitali za Rufaa za Wilaya 67 tuna mpango gani wa kuhakikisha kwamba inakuwa na vifaa vya kutosha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kusudio la Serikali ni kwamba pale miundombinu ya hospitali hizi za Wilaya zitakapokuwa zinakamilika na sisi kama Wizara pamoja na kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tumeshaanza maandalizi ya kuhakikisha kwamba hospitali hizi zitakapokamilika vifaa vitapatikana ikiwa ni pamoja na rasilimali watu. (Makofi)

Name

Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?

Supplementary Question 2

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Changamoto iliyopo Temeke na Mwananyamala inafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara, Hospitali ya Nyamiaga haina mashine ya kufulia nguo. Je, ni lini Serikali itatuletea mashine ya kufulia nguo ili kutatua changamoto hiyo? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Oliver Semguruka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa ambayo naye anaifanya katika kufuatilia masuala mbalimbali ya afya katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo Serikali tunayafanya lakini vilevile kuna mambo ambayo hivi vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya nayo inapaswa kuvifanya. Wanafanya makusanyo ya fedha na sisi Serikali tunawapelekea bajeti, ni wajibu wa Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ile na Mganga Mkuu wa Wilaya kuweka ununuzi wa mashine za kufulia ndani ya mipango yao. Gharama za mashine za kufulia sio gharama kubwa, ni vitu ambavyo Hospitali hii ya Nyamiaga wanaweza wakafanya kwa kupitia bajeti zake za ndani. (Makofi)

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?

Supplementary Question 3

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama ilivyo katika mikoa mingine, Wilaya ya Rungwe tunayo shida kubwa sana ya mashine za kuchomea taka na kuzivunjavunja ikiwemo pamoja na ukosefu wa vifaatiba ambavyo vinatakiwa kupatikana katika hospitali ile. Je, Serikali inajipangaje kutusaidia wananchi wa Wilaya ya Rungwe tuweze kupata mashine hiyo ikiwepo na mashine za X-ray za kusaidia wanawake katika Wilaya ya Rungwe, ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mbeya na nimpongeze kwa swali lake hilo ambalo ameuliza kuhusiana na masuala ya kuchomea taka na upatikanaji wa huduma za X-ray. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za uchomaji taka katika hospitali mbalimbali na sisi kama Wizara tumetoa mwongozo huo katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya na tunaendelea kufanya tafiti za teknolojia rahisi ambazo zinaweza zikatumika katika kutengeneza vichomea taka kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niiombe tu Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI na hata kupitia kwetu Wizara ya Afya tupo tayari kushirikiana nao kuwapa ushauri na huo utaalam ili sasa waweze kujenga hicho kichomea taka kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa huduma ya X-ray, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumeendelea kufanya tathmini ya uhitaji wa huduma za X-ray katika hospitali mbalimbali za Wilaya ndani ya nchi na tumetengeneza orodha ya Hospitali zote za Wilaya ambazo zinahitaji huduma hii na tumeshaanza mkakati wa uagizaji wa mashine mpya za kisasa za digital X-ray. Nimhakikishie kwamba pindi X-ray hizo zitakapofika basi na Wilaya ya Rungwe nayo tutaifikiria. (Makofi)

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na vilevile naipongeza Serikali kwa kweli kwa kuboresha huduma za afya pamoja na kwamba kazi ni kubwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nauliza kwamba tulikuwa na ICHF au CHF katika Wilaya zingine kama ilivyo Hanang’ na ilikuwa inafaidisha sana wananchi sasa nasikia kuna utaratibu wa kubadilisha utaratibu na wananchi wanateseka sasa hivi kama hawawezi kutumia CHF au ICHF, Serikali inasemaje kwa hili? Ni kweli kuna utaratibu? Na kama kuna utaratibu sasa hivi katika transition au katika muda wa mpito wananchi wanafanya nini na wananchi wa Hanang’ kwa kweli wamelalamikia hilo. (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali tulikuwa na utaratibu unaitwa CHF na katika utaratibu ule wa awali, mtu alikuwa anakata kadi anapata huduma za afya katika eneo tu ambalo ametoka, kama ni zahanati basi anapata pale kwenye ile zahanati peke yake sasa katika kile kituo ambacho yeye alikuwa amekatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumekuja na kitu kinaitwa CHF iliyoboreshwa, katika CHF boreshwa inampatia wigo wa huduma mpaka katika ngazi ya Mkoa, yanaanzia katika ngazi ya zahanati, anakwenda katika kituo cha afya, anakwenda Hospitali ya Wilaya mpaka katika ngazi ya Mkoa, haitoki nje ya pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na huu utaratibu wa CHF iliyoboreshwa unatupa gharama ya shilingi 30,000 kwa maeneo ya Vijijini na gharama ya 150,000 katika maeneo ya mjini mtu na mwenza wake na wategemezi 4 wanapata huduma zote za afya kwa gharama hiyo ambayo nilikuwa nimeisema. Kwa hiyo, utaratibu huu ndio ambao unakuwa unaendelea na mimi nipo tayari kukaa na wewe Mheshimiwa Mary Nagu kuweza kubaini changamoto zilizopo katika Wilaya ya Hanang ili tuweze kuzitatua kwa haraka. (Makofi)