Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Mto Msimbazi?

Supplementary Question 1

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali yetu kwa kutekeleza miradi mingi iliyokuja kutatua matatizo ya wananchi, hasa katika Jimbo letu la Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali nayakubali na ni ya muda mrefu. Wakati wa bajeti Mheshimiwa Matar aliiuliza Wizara ya Fedha kwa nini miradi kama hii ambayo wafadhili wako tayari kutoa pesa inacheleweshwa? Wizara ikasema, gharama hailingani na uhalisia. Je, majibu ya Serikali ambayo ime-quote gharama ile ile ya dola milioni 120 sasa wanaona gharama hizi zinaendana na wakati na zitaenda kutekelezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali kama inakubaliana nasi, mradi huu ni muhimu kutekelezwa. Kama inaendelea kusema gharama hizi ni kubwa, wanafanya mazungumzo kuja kwenye gharama halisi au wanachagua kuweka wawekezaji wa ndani ili bonde hili lipate kujengwa na wananchi walipe fidia wapate kuishi maisha bora?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, gharama hizi ndizo gharama ambazo zimeandikwa kwenye andiko. Andiko lile ni zito na kubwa sana na bado mchakato unaendelea kwa sababu, keshokutwa mimi mwenyewe nitapokea uwasilishaji wa andiko hilo kutoka kwa wadau hawa waliolitayarisha.

Mheshimiwa Mwenyeikiti, ni kitu kizuri kwa kweli na ni kitu kikubwa sana. Kwa hiyo, ndani ya Serikali lazima tupewe muda wa kuchakata ili tuweze kutoka na kitu kizuri kwa sababu kusema ukweli gharama hizi pamoja na kwamba zinaonekana kubwa, lakini pia ni lazima tuone kwamba na huu Mto Msimbazi ni mrefu, lakini pia unaweza kugeuzwa badala ya kuwa tatizo ukawa na fursa kubwa kama nilivyosema kwamba kutakuwa kuna parking, kutakuwa kuna ma-conference na vitu vikubwa vingi sana ambavyo vitajengwa kando kando ya Mto Msimbazi, lakini pia kutunza ikolojia na kuleta ladha na uzuri wa maeneo ya Mto Msimbazi kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama kwamba ni zile zile, ni kweli, bado mpaka sasa ni zile zile, lakini mchakato ndani ya Serikali unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kwamba kwa kuwa, gharama ni zile zile sasa je, Serikali iko tayari? Ni kwamba Serikali kwa maana ya uzuri wa mradi iko tayari, lakini suala la fedha ni suala ambalo pia linahusika na Wizara ya Fedha. Nasi bado tunaendelea na mchakato katika eneo letu na baadaye taarifa hii tutaikabidhi na ikibidi hata kuja kufanya uwasilisho hapa Bungeni ili Wabunge muweze kuona na pengine wananchi nao waweze kujua namna ambavyo kwa kweli Mto Msimbazi na Dar es Salaam itakavyokuwa baada ya utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba wananchi wa Dar es Salaam, kama walivyoshiriki vizuri katika uandaaji wa mradi huu, basi tuendelee kushirikiana na wawe wavumilivu kwa sababu hili jambo siyo dogo, ni kitu kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Primary Question

MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Mto Msimbazi?

Supplementary Question 2

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo haya ya Mto Msimbazi yanafanana sana na matatizo yaliyopo maeneo ya Hananasifu. Sasa je, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa World Bank wako tayari kutupatia fedha kwa ajili ya kuondoa matatizo haya ya mafuriko katika mto ule: Je, ni lini sasa Serikali itaridhia hili?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utayari wa Benki ya Dunia ni jambo moja, lakini uhalisia wa gharama pia ni jambo jingine, kwa hiyo kama Serikali siyo kwamba ni Serikali inayopokea pokea offers tu ni lazima tuangalie kwamba tunachokipokea kina tija na je gharama yake ni sahihi? Kwa hiyo, nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tuna nia ya kutekeleza mradi na andiko liko tayari na kwa kweli wadau wanaojitokeza siyo World Bank tu wako na wengine wanaojitokeza wengi lakini lazima tutafakari na kuangalia uhalisia wa gharama, Hivyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanya uwekezaji lakini kwa kuangalia uwezo wa uchumi wa nchi yetu lakini pia na aina ya msaada tunaoupokea.

Name

Yussuf Haji Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Nungwi

Primary Question

MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Mto Msimbazi?

Supplementary Question 3

MHE. YUSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika mvua za masika za mwaka jana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kwamba tayari Serikali imepata mfadhili na watajenga mto Msimbazi badala ya kuwa adhabu itakuwa ni starehe kubwa kwa sababu utakuwa ni kivutio kikubwa cha utalii kwa mkoa wa Dar es Salaam. Leo Mheshimiwa Waziri anasema bado kuna mchakato. Je, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa ina mradi wake na Serikali Kuu ina mradi wake au ni huo huo mmoja hamjakubaliana?(Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu yote kuanzia jibu la msingi na haya ya nyongeza, nimesema Serikali iko tayari na ina mpango wa kutekeleza mradi huu na ndiyo maana tumesema mradi huu utakuwa kivutio kikubwa utakayoipamba Dar es Salaam na kuwa Dar es Salaam nzuri sana kwa sababu ni mradi ambao ukisharekebisha Bonde la Mto Msimbazi kwa ukubwa wake, na kuweka parking za magari conference centers lakini pia maua na vitu kama hivyo basi maana yake ni mradi ambao utakuwa umeipamba Dar es Salaam na hivyo kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba Dar es Salaam itakuwa nzuri na Msimbazi itakuwa nzuri, bado inabaki pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumzia hapa ni kumalizia mchakato wa kutafuta fedha, offers zipo lakini kama Serikali lazima tufanye utaratibu kwa kuzingatia sheria ya misaada na mikopo ili tuweze kupata mikopo au msaada ambao una tija, hapa ndipo tunaposema gharama hizi zilizoandikwa bado ni mapendekezo, lakini kama Serikali tunamalizia mchakato wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza mradi huu. Kwa hiyo, mradi upo na utatekelezwa lakini Serikali lazima ijiridhishe na offers tunazozipewa. (Makofi)