Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. MHE. KHAMIS YAHYA MACHANO) aliuliza:- Tarehe 19 Agosti, 2019, zaidi ya wanafunzi 100 walisafiri kwenda masomoni China na India na ni ukweli kuwa elimu ya juu ni suala la Muungano:- (a) Je katika wanafunzi hao ni wangapi wanatoka Zanzibar pamoja na majina yao? (b) Je, ule utaratibu wa Zanzibar kupewa Scholarship bado unatekelezwa? (c) Je, ni lini Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia atakutana na Waziri wa Elimu Zanzibar ili kuweka utaratibu mzuri wa masuala ya elimu ya juu?

Supplementary Question 1

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichouliza Mheshimiwa, Je, Kati ya wanafunzi hao ni wangapi waliotoka Zanzibar pamoja na majina yao. Swali hili limeletwa zaidi ya mwezi mmoja na, kwa maana hiyo wizara haijawa tayari kutaka kujibu na ninaomba utumie kanuni yako swali hili lije tena. Baada ya hayo, tuendelee hivyohivyo, kwa kuwa suala hili la Muungano wala siyo hisani wala fadhila, ni la Muungano, kwa mujibu wa Katiba ambayo umeisaini wewe bwana Chenge, ukurasa mwisho 124. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo inayoshughulikia masuala yote ya elimu ya juu, Wizara ya Elimu ya Zanzibar kukosa fursa hii. Je, ni lini watakaa kuweka utaratibu huu Zanzibar vijana hawa wakapata masomo kuhusu Elimu ya Juu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tokea kuanza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kweli karibu mwaka wa nne, vikao hivyo vimefanyika mahali gani na wapi, kama Mheshimiwa Waziri ni mkweli wewe. Tuwe wakweli, hii si fadhila wala hisani, kwa mujibu wa Katiba hii? (Makofi)

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jaku kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, kwamba nafasi za ufadhili zinazotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hutolewa kwa Watanzania wote bila kujali wanatoka upande gani wa Muungano. Wakati tunatangaza nafasi hizo, kawaida hakuna sifa au hakuna hitaji la wewe kusema kwamba unatokea upande gani wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anaponitaka mimi nije na orodha ya wanafunzi wangapi wamenufaika wanaotoka Zanzibar, ananipia kazi ambayo kawaida hatuifanyi, kwa sababu sisi tunachofanya tunapopata nafasi, tunakaa na wenzetu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kupitia sifa zile halafu tunawachagua wanafunzi wa Kitanzania, bila kujali wanatoka wapi. Kwa hiyo, hatuwaambii waandike kama wanatoka Zanzibar au wanatoka Bara. Kwa hiyo, orodha ambayo ananiomba sisi hatuna! Kwa sababu hatuchukui wanafunzi kwa kuzingatia sifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimhakikishie kwamba Wizara yangu inashirikiana vizuri sana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kila wakati tunahakikisha kwamba pande zote za muungano zinapata manufaa sawa bila ubaguzi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima afahamu kwamba nafasi hizi hutolewa na wale wanaoomba wanatakiwa washindane. Kwa hiyo, mara nyingine ukisema tuanze kukaa na kusema tuanze kuchukua watu kulingana na wametoka wapi, tunaweza tukashindwa kwa sababu kule wanakwenda kushindana na wanafunzi wa nchi zingine. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba, asijenge ubaguzi kichwani, sisi hatuna ubaguzi, tunakaa na wenzetu na wala hakuna malalamiko yoyote ambayo yameshakuja kwamba kuna Wazanzibar ambao washindwa kupata nafasi hizi.