Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, ni lini Halmashauri ya Mji wa Mafinga itaingia katika mpango wa uendelezaji na uboreshaji wa Miji?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kabla ya maswali yangu mawili ya nyongeza, napenda kutoa pongezi kwa Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa barabara kati ya Mafinga na Igawa, ambayo ilikuwa imeharibika na kiasi cha kuwa chanzo cha ajiali nyingi ambazo zilipoteza maisha ya watu wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, barabara zinazopitika mwaka mzima Mafinga ni wastani wa asilimia 24 tu; na Mafinga ni kitovu cha shughuli za kiuchumi za Wilaya ya Mufindi kutokana na mazao ya misitu na hivyo kuwa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa Taifa letu. Je, Serikali, iko tayari kuiangalia Mafinga kwa jicho la huruma na kuiongezea fedha TARURA Mafinga ili angalau barabara hizi ziweze kupitika kwa mwaka mzima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri ukurasa wa 83, TARURA inasimamia wastani wa barabara zenye urefu wa kilomita 100,000 na zaidi na katika hizo, lami haizidi kilometa 1,500, changarawe haizidi kilometa 24,000, za udongo hazizidi kilometa 85,000, madaraja zaidi ya 2,000 na makalavati zaidi ya 50,000. Je, Serikali iko tayari kuiangalia TARURA na kuiongezea fedha ama kupitia mfuko wa barabara ama kutafuta chanzo chochote? Kwa sababu ndiyo ambayo inasimamia barabara nyingi zinazobeba uchumi mkubwa wa kubeba mazao, malighafi na bidhaa kutoka vijijini kwenda highway?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza bwana Chumi kwa sababu amekuwa mpiganaji mkubwa sana wa Mafinga katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, ukiangalia Mji wa Mafinga sasa unakua na eneo kubwa sana la uchumi. Ndiyo maana katika majibu yangu au majibu yetu, Naibu Waziri alizungumza kwamba Mafinga, Kasulu, Nzega na maeneo mengine ambako ile miji imechipua hivi sasa ambayo haikuwepo katika mpango wa kwanza, tunaliwekea mpango maalum. Kwa hiyo, Mheshimiwa Chumi nikuhakikishie kwamba Serikali itafanya tathmini ya kutosha nini kifanyike kwa Mafinga? Lengo ni kusaidia Mji wa Mafinga unaokua ambao vilevile unachangia uchumi hasa wa Taifa letu hili kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongeza financing katika suala zima la TARURA, ni kweli. TARURA mwanzo tulifanya tathmini, mtandao wa barabara ulikuwa ni kilomita 108,000 lakini sasa hivi tathmini ya juzi, imefika kilomita 135,000, kwa hiyo, package yake ni kubwa. Kwa kuliona hili, Serikali hivi sasa kupitia Mfuko wa Barabara inaendelea kufanya tathmini, nini kifanyike kwa lengo la kuangalia jinsi gani tuboreshe kwa ajenda kubwa ya kusaidia TARURA iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunaendelea kufanya resources mobilization kutafuta vyanzo vingine vya mapato na hasa kupitia wadau wetu wa maendeleo. Hapa niwashukuru DFID pamoja na USAID kwa kazi kubwa tunayoendelea kuifanya hivi sasa. Imani yangu ni kwamba kwa mkakati wa Serikali tunaoenda nao, huko mbele ya safari, tutahakikisha TARURA inafanya kazi vizuri kwa maslahi mapana ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, ni lini Halmashauri ya Mji wa Mafinga itaingia katika mpango wa uendelezaji na uboreshaji wa Miji?

Supplementary Question 2

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mji wa Tunduma ni sawa na Mji wa Mafinga na mji huu uko mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni sura ya nchi ya Tanzania ambayo inapitiwa na Mataifa zaidi ya nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa uboreshaji wa miji hasa kwenye miundombinu ya barabara, unatakiwa ufanyike pia katika Mji wa Tunduma: Je, Serikali imejipanga namna gani kuhakikisha kwamba Mji wa Tunduma unapata barabara bora katika mpango huu ambao utaanza mwaka 2020.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru ndugu yangu kwa swali zuri la Tunduma. Nami nikiri wazi kwamba Tunduma ni miongoni mwa miji inayokua na hata katika kutembea kwetu pale, tulitembelea maeneo ya hospitali kuangalia miradi ya maendeleo, ni kweli kuna maeneo yana changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyosema awal kwamba ni mpango wa Serikali, kwa sababu kuna ile miji ambayo ilianzishwa baada ya mpango kuanza, ambapo tulikuwa tumepata dola za Kimarekani karibu milioni 254, lakini pia kupitia mradi wa TSP tumetumia karibu milioni 840. Kwa hiyo, katika mpango wa sasa ni kwamba tutaweka Tunduma na maeneo yote yale ambayo mwanzo hayakuhusishwa katika ule mpango wa awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa ni kwamba, kama tulivyofanya katika miji yetu mikuu sasa hivi ukienda Mbeya, Tanga, Arusha, Dodoma, ukienda Babati, Iringa, Musoma, Tabora, kokote unakopita tumefanya uwekezaji mkubwa wa kujenga barabara za kisasa, kuimarisha miundombinu na tutaendelea katika hiyo miji mipya ambayo ipo Tunduma hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.