Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuza:- Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyabiasha kupitia Baraza la Uwezeshaji:- (a) Je, ni vigezo vipi vinatumika katika kutoa mikopo hiyo? (b) Je, ni wafanyabiashara wangapi ambao wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma?

Supplementary Question 1

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikia vigezo ambavyo vinatumika katika kutoa mikopo. Pia nafahamu katika maeneo yetu tunavyo vikundi vya wajasiriamali vikiwemo vikundi vya VICOBA na SACCOS. Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kufikisha elimu hiyo kwa walengwa na hasa walioko vijijini ili kuwawezesha wana VICOBA na SACCOS kunufaika na mikopo hii ambayo inatolewa na Baraza la Uwezeshaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nimekuwa nikisikia kwamba kuna Baraza la Uwezeshaji wa Taifa, napenda kujua haya Mabaraza yapo na ngazi za Mkoa, Wilaya na hadi ngazi za Kata ili wana vikundi wale waweze kuyatambua na kupata mikopo kupitia Mabaraza hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sikudhani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Sikudhani kwa jinsi ambavyo ameendelea kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wanapata manufaa ya yale yanayotendeka ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Sikudhani ni Mbunge wa Viti Maalum lakini tunaona anatetea wananchi kwa ujumla wake. Mheshimiwa Sikudhani, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nije kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, ameuliza ni njia zipi ambazo Serikali inazitumia kuhakikisha kwamba elimu hii ya uwepo wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ama fursa ambazo zinazopatikana ndani ya Taifa letu inawafikia wananchi wetu. Serikali siyo kwamba ina mikakati bali imekuwa ikifanya kwa kutumia media, tumekuwa tukitumia media mbalimbali kuhakikisha kwamba taarifa hizi za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinawafikia wananchi. Sambasamba na hilo Serikali kila mwaka tumekuwa tukitumia maonyesho mbalimbali ambapo katika mwaka wa fedha uliopita 2018 maonyesho haya yalifanyika Mkoani Mbeya lakini pia mwaka huu wa fedha maonyesho haya mwezi Oktoba yatafanyika Mkoani Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukifanya makongamano pamoja na semina mbalimbali. Katika makongamano haya tumekuwa tukishirikiana na Wakuu wa Wilaya kwenye Wilaya mbalimbali. Kupitia makongamano haya, tumekuwa tukienda na hii Mifuko yetu na kutoa elimu kwa wananchi wetu na wale ambao wanakuwa tayari basi wanapata mikopo palepale wakati wa maonyesho hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine tulio nao ni kwamba umeandaliwa Mwongozo wa kuipima Mifuko hii ni kwa jinsi gani inafanya kazi. Kipimo kimojawapo ni kuangalia ni kwa jinsi gani imetoa fedha kwa wananchi wetu au ni kwa kiasi gani imefikia wananchi wetu. Kwa hiyo, mikakati tuliyo nayo ndani ya Serikali ni mingi na Mwongozo huu utazinduliwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ameuliza Mabaraza haya yako katika ngazi zipi. Mabaraza haya yako kwenye ngazi za Halmashauri kupitia Waratibu. Tuna Waratibu mbalimbali ambao wanaratibu masuala haya ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.