Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- Michezo mingi ikiwemo mpira wa miguu inapata ufadhili sana hapa nchini kupitia kampuni mbalimbali binafsi na za Kiserikali:- Je, ni lini Serikali itahakikisha ufadhili unapatikana kwenye michezo inayohusu wanawake hususan michezo ya ngumi kwa wanawake?

Supplementary Question 1

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na jibu la msingi la Serikali, Serikali inao wajibu wa kuwekeza kwenye michezo yote ndipo wafadhili wanafuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mchezo wa ngumi kama navyoutetea hauna ufadhili wa Serikali ili kupata timu nzuri itakayotuwakilisha kimataifa. Ni lini Serikali itaandaa maeneo ya wanamichezo hawa kufanya mazoezi ili waweze kuwa vizuri na kuweza kushinda katika timu za kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika, hasa kwenye ngumi, ameonesha jitihada za kusaidia wachezaji wa ngumi kwa sasa. Serikali kwa wachezaji wa ngumi wanaume tayari wameonesha jitihada ni lini sasa watafanya hivyo kwa wachezaji wa ngumi wa kike ambao bado wako nyuma kwenye vifaa vya kufanya mazoezi ili waweze kushinda? Ahsante.

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ni miongoni mwa mapromota wanawake wachache kabisa ambao tunao nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianza na swali lake la kwanza ambapo amesema kwamba Serikali ina wajibu wa kuwekeza katika michezo yote. Ni kweli kwamba sisi kama Serikali tuna wajibu wa kusimamia lakini kazi kubwa ya Serikali ni kuandaa miundombinu na kuweka mazingira wezeshi ya kisera pamoja na sheria. Suala la ufadhili wa michezo yote nchini Tanzania ni la vyama pamoja na mashirikisho ambayo ndiyo yanasimamia michezo hiyo vilevile kwa kushirikiana na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sisi kama Serikali tunao mpango wa kuhakikisha kwamba tunafanya uwekezaji mkubwa zaidi katika michezo. Ndiyo maana umeona katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imepata fursa ya kuweza kushiriki kwenye mashindano mbalimbali na sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kwamba tunafanya ufadhili katika michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa ngumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye swali lake la pili pia ametaka kujua ni lini sasa Serikali itaanza kuweka mkakati kuhakikisha kwamba tunakuza mchezo huu wa ngumi. Kama ambavyo amezungumza ni kweli sisi kama Wizara ya Michezo kwa kipindi cha hivi karibuni tumefanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha kwanza tunaboresha mchezo huu wa ngumi na jambo la msingi ambalo tumelifanya ni kuhakikisha kwamba tunaunda Kamisheni ya mchezo huu wa ngumi. Lengo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba mchezo huu wa ngumi unapata mafanikio makubwa kitaifa na kama ambavyo tumeshuhudia kwamba ni mchezo ambao tunaamini kabisa kama uwekezaji ukifanyika vizuri utakuwa na mafanikio makubwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kwa upande wa Serikali tayari tulishaanza kuweka mikakati na matunda yameanza kuonekana ndiyo maana jana tulishuhudia wanamasumbwi watatu wamekuja hapa na mikanda ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, kama Serikali tunatambua umuhimu wa mchezo huu na tunaahidi kwamba tutaendelea kufanya uwekezaji mkubwa vilevile kwa kushirikiana na wadau. Ahsante.