Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. AUG USTINE V. HOLLE aliuliza:- Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kasulu Mjini hadi Kibondo utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Kata za Kalela, Kwaga, Lusesa, Kasangezi, Muzi pamoja na Bugaga kwa kweli barabara ya kutoka Kidahwe - Kasulu sasa ni lami. Wananchi hawa tangu uhuru sasa wamepata barabara ya lami na wana furaha kubwa sana wanaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, nini kauli ya Serikali kuhusu barabara ya kutoka Kasulu - Uvinza ukizingatia wananchi wa Kata za Lungwe Mpya na Asante Nyerere na maeneo mengine wanapata tabu sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini mipango ya Serikali kuhusu barabara ya kutoka Kitanga - Kibondo ukizingatia wananchi wa Kata za Kitanga, Kigabye na maeneo ya jirani wanapata tabu sana wanapoenda Kibondo? Nashukuru. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Vuma kwa umahiri wake, najua anawapigania sana wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maswali yake niseme kwamba tunazitazama hizi barabara alizozitaja lakini kwa sababu tumekuwa na changamoto ya ujenzi wa barabara za lami hususan kuunganisha Mkoa wa Kigoma, naomba wananchi hawa watuvumilie. Hata hivyo, niseme tu hii barabara ya kutoka Kasulu kwenda Uvinza kwa maana inaanzia pale Kanyani kwenda Kibaoni kilometa 53 tunajitahidi kuiweka barabara hiyo katika hali nzuri. Niwahakikishie wananchi wa maeneo haya ikiwemo wananchi wa Nguruka wataweza kupita vizuri.

Mheshimiwa Spika, tukikamilisha ujenzi wa barabara hii kubwa ambayo nimeitaja kwenye jibu la msingi, tutatazama namna nzuri ya kufanya ili tuone tunafanya maboresho makubwa kwenye barabara hii. Hii ni pamoja na kuiangalia kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara yake ya pili hii aliyoitaja kutoka Kitanga kwenda Kibondo ni barabara ambayo inasimamiwa na TANROADS, Mkoa wa Kigoma na ipo katika hali nzuri. Niseme tu kuna changamoto katika Daraja hili la Mto Malagarasi, eneo hili ndiyo wananchi wanapata shida kuvuka kwenda Kibondo. Nimhakikishie Mheshimiwa Vuma na wananchi wa maeneo haya kwamba mara baada ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, lipo daraja la chuma katika Mto Malagarasi, tutaangalia uwezekano wa daraja hili kulihamishia kwenye maeneo haya ili wananchi wa Kitanga waweze kupita kwenda Kibondo bila matatizo yoyote. Ahsante sana. (Makofi)