Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Primary Question

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:- Je, Serikali inasema nini juu ya ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na mbolea ambazo huwasababishia wakulima hasara?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nzuri za Serikali kutaka kuhakikisha wananchi wanapata mazao yao pindi wanapokuwa wamelima vizuri lakini napenda kujua, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inafanya utafiti wa kutosha kuhusiana na aina ya mbegu na aina ya mbolea pamoja na aina ya udongo wa sehemu husika ili wananchi waweze kulima vizuri na wasiweze kupata hasara? Katika Mkoa wangu wa Katavi, Jimbo la Kavuu mahindi yameenda vizuri na mvua hizi lakini bado kuna mdudu ambaye amekuwa akishambulia mahindi na hivyo kusababisha hasara.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingi ya Kusini Magharibi imekuwa ikitajwa kama ni mikoa ya uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mpunga na maharagwe.

Je, Serikali ina mkakati gani hususan katika Mkoa wa Katavi kuhakikisha kwamba inafanya utafiti na ku-introduce zao la biashara kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi ili waweze nao kutoka kwenye masuala ya mazao ya chakula waende sasa kufanya biashara katika mkoa huo? Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba watu wao wanapata mazao ya kibiashara?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali kwanza tuna Kituo chetu cha Utafiti cha Mlingano Tanga ambacho tumekipa jukumu mahsusi kwa ajili ya utafiti wa udongo kuangalia afya ya udongo na tabaka la udongo ili kufahamu kwamba udongo wa sehemu husika unakubali mazao gani, una upungufu wa virutubisho vya ardhi vya mbolea kiasi gani ili sasa kumwelekeza mkulima kulima kulingana na ikolojia ya eneo lake na mazao yanayokubali kutokana na ardhi ile.

Mheshimiwa Spika, kazi hiyo ya awali tumeshamaliza kwenye mikoa zaidi ya 16 na sasa hizi pia tumetambulisha maabara yetu kama pale SUA na Chuo cha Kibaha (TARI) kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, niwahamasishe wakulima wote kuchukua nafasi hasa kwenye kilimo cha biashara ni vizuri kufanya utafiti wa udongo kabla ya kulima kwa sababu ardhi imeshachakaa sana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mkakati wa Serikali tuliokuwa nao kwa ajili ya kutambulisha mazao ya biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu hususan katika Mkoa huu wa Katavi. Kwanza hili ni swali zuri sana na ni mkakati wa Serikali sasa hivi kuwatengenezea wakulima kuwa na kiiunua mgongo wakati wanapofikisha miaka zaidi ya 60 kwa sababu kuendelea kulima mazao muda mfupi mahindi na mpunga maana yake ni kuwalazimisha wakulima kulima mpaka kufa. Katika mipango hii ya Serikali katika Mkoa wake wa Katavi, mwaka huu tumeshaanza kuzalisha miche zaidi ya 600,000 ya korosho na tumeshagawa sasa hivi katika Wilaya ya Tanganyika miche zaidi ya 250,000 na tarehe 8 mwezi huu tunakwenda kugawa miche iliyobaki ya korosho zaidi ya 350,000 katika Wilaya zote za Mkoa wa Katavi ili sasa kutambulisha na kuhamasisha wakulima hawa wakalima mazao muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwaka huu temegawa zaidi ya miche 800,000 ya kahawa katika Mkoa huo huo wa Katavi na mwaka huu unaokuja katika bajeti tumepanga kuzalisha miche 1,000,000 ya kahawa, miche 1,000,000 ya korosho na miche 1,000,000 ya maparachichi ili kwenda kuipanda katika Mkoa huo wa Katavi. Nakushukuru sana.