Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEY G. MASSAY (K.n.y. MHE. QAMBALO W. QULWI) aliuliza:- Wakulima wa Bonde la Eyasi wanategemea kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia chemchem za Qangded; na kutokana na kupungua kwa kiasi cha maji katika vyanzo hivyo wakulima wengi wanashindwa kuzalisha:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vyanzo mbadala kama mabwawa na visima virefu ili kilimo katika bonde hilo kiwe endelevu?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEY G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri yanasema fedha hazipatikani na zitengwe kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ya Karatu; na kwa sababu ukiangalia mapato ya Halmashauri hayana uwezo wa kujenga hata bwawa: Je, Serikali haioni sasa itumie namna mbadala kutokana na hali hii ili kusaidia watu wa Bonde la Eyasi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Mbulu zilikuwa Wilaya moja na Bonde la Eyasi ni sawasawa na Bonde la Bashai: Je, kuna mpango gani pia wa kusaidia Bonde la Bashai kulipatia fedha ili skimu hii ipate kuendelea?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Flatey Massay anasema kwamba Serikali ya Halmashauri ya Wilaya haina fedha ya kuweza kujenga hili bwawa wala miundombinu mingine mbadala wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali tutaendelea kutenga bajeti ile ya kiserikali kutoka Serikali Kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, lakini kama tulivyoelekeza, naye mwenyewe anajua. Hili Bonde la Eyasi kwenye kilimo tu cha vitunguu ndiyo linachangia mapato zaidi ya asilimia 33 ya Halmashauri hiyo ya Karatu, lakini haipeleki Halmashauri hiyo ya Karatu hata senti tano kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha vitunguu katika bonde hilo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kama Serikali tumeelekeza watenge kwenye mapato yao ya ndani asilimia 20 ili kwenda kunenepesha ng’ombe yule wanayemkamua kwenye vitunguu ili waweze kukamua zaidi siku zijazo. Hatujasema kwanza hicho ni chanzo pekee cha kuendeleza huko, hapana. Hicho ni kimojawapo, ndio maana nimesema kwenye ile programu ya Jenga, Endesha na Kabidhi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Rasilimali pia wanaruhusiwa kwenda kuchukua mkopo. Tutaenda kujenga hiyo miundombinu baada ya kuiendesha halafu baadaye tutakabidhi baada ya mapato hayo kuisha. Pia tutaendelea kutenga kwenye bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, skimu hii iliyokuwa katika Wilaya ya Jimbo la Mbulu pia utaratibu utakuwa ni huo huo na ombi lake nimelipokea, ni vizuri alete sasa hilo andiko na tutatuma Tume ya Taifa ya Umwagiliaji waende huko wakafanye tathmini na kuangalia mahitaji, baadaye tutaingiza kwenye bajeti kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa skimu hiyo.