Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:- Sera ya cost sharing ilianzishwa ili kuisaidia Serikali kibajeti katika maeneo ya afya na elimu, hadi leo ni bayana kuwa sera hii imeshindwa na hatimaye Serikali kurejea tena katika kugharamia Elimu ya Msingi na Sekondari:- (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Elimu ya Tanzania ambayo imeporomoka sana katika shule za Umma inakuwa yenye ubora unaotarajiwa? (b) Je, Serikali inafanya nini kuhusu madai ya stahiki ya walimu ambazo hazijalipwa kwa muda mrefu sasa?

Supplementary Question 1

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kwa bahati mbaya tu kwamba Serikali inatoa majibu na takwimu ambazo haziakisi ukweli. Katika jibu la Mheshimiwa Waziri, hizi takwimu alizozitoa pia nazo haziakisi ukweli kwa sababu ukikokotoa kiasi cha takwimu anazozitoa na ukilinganisha uhitaji ulivyo inaweza kukupa jibu ya kwamba elimu yetu inaporomoka badala ya kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, anaposema Serikali imetoa shilingi bilioni 56.05 katika shule 588, kati ya shule 17,174 maana yake wamehudumia shule 3% tu. Sasa ukiangalia kama hapo takwimu hii inakwamba elimu inakua ama inaporomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule zetu zina hali mbaya sana na nina mfano halisi ambao uko mita 1,000 kutoka majengo ya Bunge, Shule ya Msingi Medeli, hii shule haina vi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lucy, naomba uulize swali tafadhali. Naomba uulize maswali yako.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala ni sensitive kidogo, tafadhali naomba takwimu kidogo.

NAIBU SPIKA: Aaah, sasa siwezi kukupa dakika zako. Swali lako peke yake ni dakika sita. Sasa ukitumia dakika mbili kwenye swali moja la nyongeza maana yake muda wako umekwisha tayari, ndiyo maana nakukumbusha uulize swali.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi katika takwimu hizo ambazo unaziona kwamba 3% tu ndiyo imehudumiwa: Je, mazingira haya duni ambayo yanazikabili shule zetu, elimu itakuwa inakua ama inaporomoka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Madai ya walimu ni moja kati ya mwarobaini muhimu sana wa kutanzua kuporomoka kwa elimu ya Tanzania. Katika hili naomba nimwombee dua njema mdogo wangu Mwalimu Hilda Galda John Bura aliyefariki tarehe 05 na tukamzika ambaye naye amefariki akiwa anaidai Serikali madai haya haya ya walimu. Je, kwa takwimu hizi za shilingi bilioni 15.07 alizotoa Mheshimiwa Waziri, ni asilimia ngapi ya madai yote ya waalimu?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu takwimu ninazozitoa kwamba haziakisi hali halisi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu hizo nilizotoa ndiyo takwimu rasmi. Pia shule ambazo tumeweza kujenga na kuboresha miundombinu ni katika kipindi fulani. Nimeweza kuainisha kwamba ni kutoka mwaka 2017 mpaka sasa, haimaanishi kwamba huko nyuma hakukuwa na kitu ambacho kimefanyika, lakini haimaanishi kwamba siku za usoni hatutafanya kitu kingine. Kwa hiyo, shule 588 katika kipindi cha miaka mitatu siyo kitu kidogo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu kwamba Serikali itaendelea kuboresha miundombinu kadiri ya upatikanaji wa fedha utakaporuhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu malimbikizo ya madeni ya walimu naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza madeni hayo. Kwa sasa tunachojaribu kufanya ni kuhakikisha kwamba madeni mapya hayatokei. Tunalipa stahiki za walimu pale zinapohitajika.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nimesimama hapa kuweka msisitizo kwamba Serikali inafanya kazi vizuri sana katika kuhakikisha kwamba inaboresha Sekta ya Elimu. Hii takwimu ambayo imetolewa hapa ni mfano wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo. Haijajumuisha shilingi bilioni 29 ambazo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilizitoa kwa ajili ya kukamilisha maboma; haijajumuisha shughuli ambazo Halmashauri zetu katika bajeti zao zinatenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Lucy Magereli kwamba Serikali iko vizuri, mwenye macho haambiwi tazama. Ukienda unaona hata shule kongwe zilivyoboreshwa, zinapendeza, zilikuwa majengo mabovu. Kwa hiyo, watupe muda, Serikali tutaendelea kufanya kazi yetu vizuri.