Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:- Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kwenye suala la ubakaji (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho yaliyofanywa mwaka 2017 yote yana lengo la kukomesha vitendo vya ubakaji wa watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi (kifungo miaka 30) na watoto chini ya miaka 10 (kifungo cha maisha):- (a) Je, tokea kupitishwa kwa sheria hii (SOSPA) na marekebisho yake, ubakaji umepungua au kukoma hapa nchini? (b) Je, kama bado changamoto ipo Serikali ina mpango mkakati gani mpya katika kupambana kutokomeza ubakaji Tanzania?

Supplementary Question 1

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jitihada inazozichukua katika kulipoteza hili suala baya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza, mwaka jana nilizungumza hapa kwamba iwapo elimu tosha itatolewa basi ripoti hizi zitazidi. Kweli Mheshimiwa Waziri amethibitisha, hivyo nawapongeza sana kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kujua hii idadi kubwa ambayo imeongezeka baada ya wananchi kuhamasika na kutoa ripoti, je, ni wangapi kati ya hao wameweza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wangapi wametiwa hatiani na kuchukuliwa hatua zinazostahiki? Siyo lazima mnijibu sasa hivi lakini majibu nayataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunajua kabisa vitendo hivi vinafanywa miongoni mwa jamii tunazoishi, ni miongoni mwa wanaume tunaoishi nao wakiwemo babu zetu, baba zetu, waume zetu, wajomba zetu na wengine wanaofanana na hao. Kwa nini Serikali haiji na mpango mbadala wa kutoa ruhusa kwenye jamii ili kuwatambua hawa watu ambao wanajulikana wana vitendo hivi kama ambavyo wanatambuliwa wabakaji, wezi, wavuta unga na wavuta bangi; ili jamii yetu sasa iweze kuwajua na wazazi pamoja na watoto wetu waweze kujitenga na watu hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio haya ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na mara nyingi inakuwa ndani ya familia. Sisi kama Wizara tumeendelea kuelimisha jamii na tunawashukuru sana wenzetu wa Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Mahakama, wamekuwa wanatoa ushirikiano mkubwa sana. Matukio mengi yanashindwa kufika mbali kwa sababu ushirikiano umekuwa ni mdogo ndani ya familia kwenda kutoa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hapa sina takwimu ambazo zinaonesha matukio ni mangapi na kiasi gani yamehukumiwa, lakini kwa taarifa chache ambazo ninazo, ni matuko machache sana ambayo yanafika mwisho kwa sababu tu familia zimekuwa hazitoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Mahakama ili matukio haya yaweze kufika mwisho. Kwa hiyo, nitoe rai kwa jamii kutomalizana na haya matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto majumbani na badala yake waruhusu mkondo wa sheria uweze kufika mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili, katika nchi ambazo zimeendelea, kuna kitu kinaitwa Sexual Offender Register. Wale watu ambao wamehukumiwa kutokana na makosa haya ya ukatili wa kijinsia wanatambulika wapi wanakaa, wapi wanafanya kazi na akihamia sehemu mpya watu wote wanaweza wakamfahamu. Kwa hiyo, kwa sasa Serikali hatuna utaratibu huo, lakini ni wazo ambalo tunaweza tukalipokea na kuweza kuliangalia ni jinsi gani ya kulifanyia kazi.