Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:- Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) pasipo kulipwa fidia:- Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kulipa fidia kwa wannachi hao?

Supplementary Question 1

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, fedha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja ya malipo ya shilingi bilioni 3 ni ile ambayo inaenda kulipwa kule Kilwa Masoko, Rasi Mshindo na Navy Command. Kuna maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi baadhi ya wananchi wameshafariki dunia na Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa kwa fedha za ndani ikionyesha kwamba wananchi hawa tayari wamedhulumiwa na hawana chao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali utuambie ni kwa nini basi mmechukua muda mrefu hamtaki kuwalipa wananchi hawa ili hali mnaenda kutekeleza miradi mikubwa ndani ya nchi kwa fedha za ndani? Lini fedha za wananchi hawa zitapatikana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 ilieleza wazi kuna maeneo kadhaa ya Jeshi yaliyoorodheshwa ambapo wananchi wanadai fidia na Serikali ikaahidi kwamba itaendelea kulipa. Ukiangalia bajeti iliyopita shilingi bilioni 27 fedha hazikutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie bajeti yake ya kesho anawaambia nini wananchi hawa wanaolalamika kwa muda mrefu, wamekata tama na wengine wameshafariki na lakini hawana mategemeo ya kulipwa fedha zao? Naomba Waziri atuambie waziwazi wananchi hawa ambao wamekata tamaa, wanyonge hawa na ninyi ndiyo watetezi wa wanyonge watapata lini? Naomba majibu ya kweli.

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdalah Salim, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba shilingi bilioni 3 zilizotolewa ni kwa ajili ya Rasi Mshindo kule Kilwa. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya fedha tulizoidhinishiwa bajeti iliyopita shilingi bilioni 20.9 ukiacha shilingi bilioni tatu ambazo zimeshalipwa shilingi bilioni 16 zimeshatengwa na kazi inayofanyika sasa hivi ni uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukichukua zile shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni 16 utaona shilingi bilioni 19 zitatolewa katika bajeti hii ambayo tunamalizia. Kwa hiyo, hatuna shaka kwamba baada ya uhakiki maeneo mengi haya yatalipwa.

Kuhusu bajeti ijayo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira. Ukweli ni kwamba kama tutafanikisha kulipa shilingi bilioni 19 kati ya shilingi bilioni 20 zilizotengwa katika bajeti tunayomalizia basi bila shaka kwa sehemu kubwa tutakuwa tumetimiza ahadi zetu.