Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:- Mkoa wa Katavi unapata mvua za masika kuanzia mwezi Septemba na Oktoba lakini mara nyingi pembejeo zimekuwa zikichelewa kupelekwa wakati mwingine hadi mwezi Novemba:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kwa wakati pembejeo Mkoani Katavi?

Supplementary Question 1

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, ninayo maswali maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja unatumika tu kwa mbolea za DAP na UREA. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitumie mfumo huu kwa kuagiza mbolea nyingine za NPK, CAN, SA na pembejeo nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi ni umbali wa kama kilimita 1,500 kutoka Dar es Salaam, kwa hiyo, mbolea inaposafirishwa na magari inakuwa na bei juu zaidi.

Ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kusafirisha mbolea hiyo kwa njia ya treni ili mkulima wa Mkoa wa Katavi apate bei nafuu ya mbolea?

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Taska Mbogo alitaka kujua kwa nini Serikali tusitumie Mfumo huu wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) kwa mbolea zingine kama NPK, CAN na SA. Kwanza, mfumo huu tumeanza kuutumia mwaka jana na umeonyesha matokeo mazuri. Tusingeweza kuingiza mbolea zote kwa wakati mmoja lakini baada ya mafanikio tuliyoyaona katika mfumo huu, mwaka huu tumeshaanza kuutumia mfumo huu kwa ajili ya mbolea ya NPK kwa wakulima wa tumbaku na sasa tutaendelea na utaratibu ili kuingiza mbolea tajwa, viuatilifu na pembejeo zingine katika mfumo wa BPS ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anasema kwa sababu Mkoa wa Katavi uko mbali na Dar es Salaam, ni vizuri tungesafirisha mbolea hizi kwa njia ya treni ili kupunguza gharama za usafiri. Tunachukua mawazo haya na tulishayafanyia kazi, tangu mwaka jana kama nilivyosema hii mbolea ya NPK tuliisafirisha kwa kutumia treni na gharama za usafiri zilishuka na mbolea hii kufika kwa wakulima kwa wakati. Mawazo yake tunayachukua ili tuyahamishie katika mazao mengine. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tayari tumeshalielekeza Shirika letu la Reli Tanzania ili kutoa kipaumbele kwenye kusafirisha bidhaa ya mbolea ili kushusha gharama za usafiri.

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:- Mkoa wa Katavi unapata mvua za masika kuanzia mwezi Septemba na Oktoba lakini mara nyingi pembejeo zimekuwa zikichelewa kupelekwa wakati mwingine hadi mwezi Novemba:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kwa wakati pembejeo Mkoani Katavi?

Supplementary Question 2

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima na wanaishi maeneo ya vijijini. Hawa wafanyabiashara aliowataja Mheshimiwa Naibu Waziri wenye makampuni wanaonunua mbolea hizi, wamekuwa wakinunua na kuziweka mjini na inawapasa wakulima sasa watoke vijijini kwenda kununua hizo mbolea mjini kitu ambacho kimekuwa kikiwasababishia gharama za mbolea kupanda sana? Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba mbolea hizi zinapatikana kwenya Kata au Tarafa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe tuna maghala na maeneo mengi ya Njombe kuna maghala kwenye Kata hizi. Je, Serikali ina mpango gani ili kuhakikisha hawa wafanyabiashara wanapeleka mbolea hizi kwenye Kata ili gharama za usafirishaji ziweze kupungua kwa wakulima? Ahsante sana.

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Hongoli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakulima wengi wanaishi vijijini na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tumeshayaelekeza makampuni yote yanayoingiza mbolea hapa nchini na wasambazaji wawe na mawakala kila Mkoa
na Wilaya na pia wawe maghala ili kuwezesha mbolea hizi zinapoingia Dar es Salaam kufika kwenye mikoa yote inayotumia mbolea kwa wingi. Pia tumevielekeza Vyama vya Msingi vya Ushirika na Vyama Vikuu, kuwa mawakala kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwenye Kata na Vijiji katika Mikoa na Wilaya zinazolima mazao mbalimbali.