Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asha Mshimba Jecha

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:- Tanzania imebarikiwa kuwa na Ukanda wa Bahari na Maziwa. Je, wananchi wa maeneo hayo wameandaliwaje kufaidika na rasilimali zinazopatikana katika Ukanda wa Bahari na Maziwa?

Supplementary Question 1

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina suala moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango mizuri ya Serikali lakini bado wavuvi wana hali ngumu, uduni wa vifaa, utaalam na kadhalika. Je, ni lini Serikali itaanzisha vyuo vya uvuvi vingine kwa sababu navyofahamu chuo kilichopo ni kimoja tu lakini hata wahitimu wake hawapati nafasi ya kuajiriwa pamoja na kwamba tumezungukwa na ukanda mkubwa wa bahari na maziwa. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwatumia wataalam wanaomaliza katika chuo hicho lakini pia kuanzisha vyuo vingine kwa lengo la kuwanyanyua wavuvi ili waweze kuwa na tija na bahari na maziwa? Ahsante.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili mazuri sana ya nyongeza ya Mama yangu Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali tunao mpango wa kuhakikisha tunafungua vyuo vingine. Hapa karibuni tumefungua chuo cha uvuvi katika Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara Mikindani, Chuo cha FETA ambacho kinafanya kazi ya kutoa elimu. Mipango mingine ya Serikali ni pamoja na kuboresha chuo chetu kilichopo pale Pangani maarufu kama KIM kwa kushirikiana na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Halmashauri ya Pangani kwa lengo la kuhakikisha wananchi hasa vijana walio wengi wa maeneo haya ya ukanda wa bahari wanapata elimu. Kwa upande wa Ziwa Victoria chuo chetu kilichopo katika Wilaya ya Rorya pale Gabimori na chenyewe tunakwenda kukiongezea nguvu ili kusudi kitoa elimu zaidi kwa wananchi wengi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza mipango yetu tuliyonayo ya kuhakikisha wale wataalam wanaotoka katika vyuo hivi wanakwenda kupata kazi na kuisaidia jamii yetu. Katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kuwa Serikali inao mpango wa kufufua Shirika letu la Uvuvi la TAFICO na tayari tumeshalifufua, hivi sasa tunakwenda katika hatua ya kununua meli. Tayari tumepata msaada kwa maana ya grants kutoka Serikali ya Japan wa takribani bilioni nne ambazo tunakwenda kununua meli na kutengeneza miundombinu ya kuhifadhia samaki katika eneo la ukanda wa pwani. Hii ni chachu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wale wengi wenye utaalam wataajiriwa na mashirika haya.

Vilevile tunao mpango wa kuhakikisha wanajiajiri wao wenyewe kwa kufanya kazi za uvuvi endelevu wa kisasa na vilevile ufugaji wa samaki.

Name

Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Primary Question

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:- Tanzania imebarikiwa kuwa na Ukanda wa Bahari na Maziwa. Je, wananchi wa maeneo hayo wameandaliwaje kufaidika na rasilimali zinazopatikana katika Ukanda wa Bahari na Maziwa?

Supplementary Question 2

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini Serikali sasa itahakikisha kwamba bandari ya uvuvi inajengwa ili fursa ya uvuvi wa bahari kuu iweze kutumika vizuri sana? Ahsante.

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la ndugu yangu Mbunge wa Mafia, jirani yangu, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni lini bandari itajengwa. Hivi sasa tuko katika kumalizia mchakato wa upembuzi yakinifu wa eneo itakapokwenda kujengwa bandari ya uvuvi. Tayari mkandarasi huyu kupitia pesa zetu wenyewe, pesa za ndani tumeshamlipa na anamalizia kazi ya kutuelekeza mahali gani katika ukanda wetu wa pwani tutakwenda kujenga bandari ya uvuvi.

Mheshimiwa Spika, habari njema zaidi, nadhani wote tumemsikia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa katika Mei Mosi pale Mbeya ameeleza juu ya nia njema ya nchi rafiki ya Korea ambapo wameonesha nia ya kutaka kushirikiana nasi katika kwenda kujenga bandari hii ya uvuvi.

Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla kwamba nia yetu hii itakwenda kutimia na hatimaye kuweza kupata faida ya uvuvi katika eneo la bahari kuu.