Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO (K.n.y. MHE. ESTER A. BULAYA) aliuliza:- TANESCO Mkoa wa Mara katika zoezi la kupeleka umeme vijijini walipitisha nguzo za umeme kwenye maeneo ya watu katika Kijiji cha Nyabeu, Kata ya Guta na uthamini ulifanyika na iliahidi malipo kufanyika lakini hadi leo hawajalipwa na badala yake wanaambiwa maeneo hayo ni ya TANESCO:- (a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao fidia stahiki? (b) Je, ni kwa nini TANESCO inamiliki maeneo kabla ya kulipa fidia?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa sasa tunajua kwamba tuna mradi wa REA ambao ndiyo umejielekeza kupeleka umeme vijijini. Katika Kijiji cha Sazira katika Jimbo la Bunda Mjini ambalo lina Vitongoji vitatu cha Nyamungu, Wisegere na Kinamo havijawahi kupitiwa na mradi huu wa REA phase I, phase II na hata phase III. Sasa ningependa kujua hawa wananchi wa Kijiji cha Sazira ni lini watapatiwa umeme ili na wenyewe waweze kupata umeme katika shughuli zao za kimaendeleo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Mji wa Tarime pia tumepitiwa na umeme wa REA ambao unapita kwenye aidha Kijiji sehemu ndogo tu au kata. Ningependa kujua maeneo ambayo yana Taasisi kama sekondari, zahanati au vituo vya afya na shule ya msingi kama vile Kitale tuna Kijiji cha Nkongole ambacho kina hizo Taasisi zote, Kenyamanyori Senta tuna Kibaga ambayo ina mgodi pale haijapitiwa na umeme wa REA. Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba inapeleka huu umeme wa REA kwenye yale maeneo ambayo hayajaguswa kabisa na Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kwamba ungeweza kwenda Tarime kujihakikishia hayo maeneo ambayo kila siku nayauliza hapa? Ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameulizia Kijiji cha Sazira ambacho kipo Bunda Mjini ambacho kina vitongoji vitatu na hakina umeme. Kama ambavyo tumepata kujibu maswali hapa ya msingi kwamba mpango wa Serikali ni kupeleka umeme vijiji vyote. Kwa sasa tuna mradi huu unaoendelea wa REA awamu ya tatu ambao unahusisha vijiji 3,559 lakini ukichanganya na miradi mingine yote ya Ujazilizi, BTIP tunatarajia kufikisha umeme ifikapo Julai, 2020 kwa vijiji 9,299.

Kwa hiyo kijiji ambacho amekitaja kwenye Wilaya ya Bunda Mjini hapo vipo katika mpango wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao utaanza Julai, 2019 na kukamilika 2021. Kwa hiyo niwatoe hofu tu wananchi wote nchi nzima, mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kupeleka umeme katika vijiji vyote nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameulizia suala la Jimbo lake la Tarime; ni kweli niliahidi kutembelea Jimbo hilo kama utaratibu wetu ndani ya Wizara, lakini nitazingatia angalizo lako kwamba kwa ruhusa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini nimtoe hofu tu Mheshimiwa Esther kwamba katika maeneo ambayo ameyataja na hasa Taasisi za Umma, Wizara imetoa maelekezo mahususi na naendelea kurejea hayo maelekezo kwamba Taasisi za umma ni moja ya kipaumbele katika kuzipelekea umeme iwe shule ya msingi, sekondari, kituo cha afya au miradi ya maji.

Kwa hiyo naomba niwaelekeze Wakandarasi kuzingatia maelekezo hayo na Mameneja wote wa TANESCO na wasimamizi wa miradi hii ya REA kwamba umeme ufikishwe kwenye Taasisi za Umma ili kuboresha utoaji wa huduma ambazo zinatokana na hizo Taasisi za umma.

Mheshimiwa Spika, katika haya maeneo aliyoyasema Mheshimiwa kwanza mojawapo lipo katika REA awamu ya tatu, mradi unaoendelea na Mkandrasi Derm yupo, anaendelea vizuri na ni moja wa Wakandarasi ambao kwa kweli wanafanya kazi vizuri na nimhakikishie tu mpaka Juni, 2019 hii miradi itakuwa imekamilika. Ahsante.