Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nuru Awadh Bafadhili

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:- Katika kipindi cha miaka ya 1970 wakati wanafunzi wakienda likizo walimu walikuwa wakienda katika vyuo mbalimbali vilivyokuwa jirani na wilaya zao ili kupewa mafunzo au kupigwa msasa (refresher courses) kiasi kwamba walimu walikuwa wanapata ari ya kufundisha vizuri:- Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha utaratibu huo kwa walimu kupigwa msasa?

Supplementary Question 1

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mbali na hayo masomo yaliyokwishafundishwa kuna somo la TEHAMA ambalo sasa hivi linafundishwa katika shule mbalimbali lakini kuna baadhi ya walimu katika shule za msingi hawana ujuzi wa kutumia kompyuta. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwapa mafunzo walimu hao ili tuendane na wakati huu wa utandawazi na digitali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa walimu wanafanya kazi zao vizuri na tunastahili kuwapa motisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa ile Teaching Allowance kama walivyowapa Wakuu wa Shule pamoja na Waratibu ili nao waweze kuipenda kazi yao na kupata morali ya kufundisha?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nuru Awadh, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuwajengea walimu uwezo katika masuala ya TEHAMA, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa TEHAMA ni kati ya maeneo mapya ambayo lazima walimu wote wajengewe uwezo kwa sababu katika enzi tulizopo sasa TEHAMA ni moja ya vitu muhimu katika elimu. Kwa hiyo, katika mipango ya Serikali TEHAMA ni moja kati ya maeneo muhimu ambayo walimu watajengewa uwezo na hili litafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la motisha, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya walimu kadiri ya uwezo utakavyoruhusu. Siku za mbele hata masuala ya motisha ni moja kati ya masuala ambayo yanaweza yakaangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Naibu Waziri wa Elimu, naomba nitumie fursa hii vilevile kuwatakia kila la kheri vijana wetu 91,440 wa Kidato cha Sita na wale 12,540 wa Vyuo vya Ualimu ambao leo wanafanya mitihani yao ya mwisho. Hata hivyo, nitoe rai kwao kwamba wafuate sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza mitihani na kamwe wasije wakajihusisha na vitendo vya wizi na udanganyifu katika mitihani.