Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:- Jimbo la Babati Vijijini linakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya mawasiliano ya simu hasa katika Vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso ambako hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ya simu:- Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo katika maeneo ya vijiji husika?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo lililoko Babati Vijijini ni tatizo pia lililoko Kiteto, Vijiji vya Makame, Ishkribo, Asamatwa, Ngaboro, ni lini sasa vijiji hivi vitaunganishwa pamoja na hivi Vijiji vya Endagwe, Hoshan, kwa ajili ya kufanya tathmini ili wananchi wapate huduma ya mawasiliano?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kijiji cha Landanai kilichoko Simanjiro na Kijiji cha Ngage, ni vijiji ambavyo vina idadi kubwa ya watu lakini mpaka sasa vijiji hivi havijafanyiwa uthamini kwa ajili ya kupata mawasiliano hayo. Ni lini sasa Serikali itapeleka huduma hii Landanai?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Gidarya, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kiteto alivyovitaja, bahati nzuri vimekwishaletwa mezani kwangu na Mbunge wa Kiteto, kupitia Chama cha Mapinduzi kwamba havina mawasiliano na tumekwishaviingiza kwenye orodha ya vijiji vitakavyopelekewa huduma ya mawasiliano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshauri tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi vijiji alivyovitaja vitapepelekewa mawasiliano na vijiji vingine hivyo vyote alivyoviulizia Mheshimiwa Mbunge, tayari ninayo orodha yake nililetewa na Mbunge wa jimbo husika. Nimhakikishie tu Mheshimiwa tukitoka hapa tunaweza kuwasiliana ukaangalia orodha ya vijiji hivyo kuona kama vimeshaingizwa au la, kwa sababu nina hakika vyote vimeshaingizwa.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:- Jimbo la Babati Vijijini linakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya mawasiliano ya simu hasa katika Vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso ambako hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ya simu:- Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo katika maeneo ya vijiji husika?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kabla sijauliza swali naomba nikutakie heri ya Pasaka kwa niaba ya Warombo wenzangu wote.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema kwamba kuanzia tarehe 1 Mei, 2019 kutakuwa na usajili mpya wa laini zote kwa kutumia alama za vidole. Ameendelea zaidi kusema kwamba hakutakuwa na ruhusa ya kumiliki zaidi ya laini mbili mpaka ruhusa maalumu ya maandishi. Mheshimiwa Waziri anafahamu kuna maeneo mengine laini hazipatikani, kuna maeneo Vodacom ipo lakini Airtel haipo. Sasa mkifanya hivyo hamtaona kwamba mtawatesa wananchi ambao huduma za baadhi ya laini hazipatikani katika maeneo yao?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la usajili kuanzia tarehe 1 Mei, 2019. Ni kweli tumezielekeza kampuni za huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi kuanza sasa utekelezaji wa kusajili kwa kutumia alama za vidole na zoezi hilo litaanza kuanzia tarehe 1 Mei, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa ruksa yako tutaomba sasa Bunge lituruhusu tulete Madawati Maalumu ya watoa huduma ili Waheshimiwa Wabunge wafanye usajili wao wakiwa humu ndani.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote kwamba hakuna sehemu ambako nilizungumza kwamba kila Mtanzania atakuwa na laini moja tu ya simu, hapana. Kilichozungumzwa na nilichokizungumza na walikuja kufafanua wenyewe baadaye ni kwamba tunatamani kila Mtanzania awe na laini moja ya simu kwa mtandao mmoja, akitaka laini nyingine, kwa sababu possibility ipo, mtu unaweza ukawa unatumia Tigo lakini ukataka Ipad yako itumie Vodacom, tunaruhusu, useme, lakini tunaepuka utitiri wa laini nyingi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wenyewe ni mashahidi mnaombwa fedha kila siku, tuma kwa namba hii, tuma kwa namba hii, hizo ni laini ambazo hazina tija na zinatuumiza sana Watanzania. Tulizungumza kwamba mtu awe na laini moja kwa mtandao mmoja, Vodacom moja, Tigo moja, Airtel moja na kadhalika.

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Primary Question

MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:- Jimbo la Babati Vijijini linakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya mawasiliano ya simu hasa katika Vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso ambako hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ya simu:- Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo katika maeneo ya vijiji husika?

Supplementary Question 3

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, naomba nirejee katika swali la msingi, siko katika mambo ya laini ya Mheshimiwa Selasini.

SPIKA: Uliza, uliza.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo Babati Vijijini yanafanana moja kwa moja na yaliyopo katika Halmashauri ya Chalize. Nimemwandikia sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake lakini utekelezaji umekuwa ni wa taratibu sana. Sasa kwa kuwa jambo hili nimeshamwandikia Mheshimiwa Waziri, naomba anijibu wamefikia wapi juu ya matatizo ya mawasiliano katika Kata ya Kiwangwa, Msata na Lugoba kama ambavyo tumeelekezana? Ahsante sana.

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Vijiji vya Kiwangwa katika baadhi ya maeneo yana tatizo la huduma ya mawasiliano lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo lake analolitaja la Kiwangwa linahitaji kuongezewa nguvu kwenye mnara wa mawasiliano ulioko pale. Kwa hiyo, namshauri aje tuonane baadaye tuangalie vijiji vingine ambavyo tumeviingiza kwenye mpango wa kupelekewa huduma na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.