Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003, Dagaa wanapaswa kuvuliwa kwa wavu wenye matundu mm 8 – mm10, lakini sheria hii haijazingatia aina tofauti za dagaa:- Je, kwa nini Serikali isifanye utafiti utakaoainisha matumizi ya nyavu kutegemea aina ya dagaa wanaopatikana kwenye Ziwa husika?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nitumie fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake na nimshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa anautoa kwa masuala ya uvuvi. Nina maswali mawili ya nyongeza; la kwanza uvuvi wa dagaa wanavuliwa kwa kuchotwa, kwa hiyo isitegemee kwamba wategemee dagaa wale wanase kwenye nyavu, ndio maana ni muhimu angalau matundu yake yawe madogo kidogo. Sasa kwa kuwa dagaa wanaopatikana Ziwa Victoria hawatofautiana sana na dagaa wanaopatikana Bahari ya Hindi na natambua kuna mchakato wa kufanya utafiti kwenye Bahari ya Hindi ili dagaa wanaovuliwa kwenye Bahari ya Hindi wavuliwe kwa nyavu za milimita sita na kuendelea. Je, Serikali haioni sababu sambamba na utafiti utakaofanyika Bahari ya Hindi ufanyike vilevile na uvuvi utakaofanyika Ziwa victoria kwa dagaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wavuvi wa Ukerewe wa samaki aina ya gogogo au ngere wanapata bugudha sana wakati wanavua samaki wale kwa kisingizio kwamba sheria hairuhusu, lakini mazingira ya uvuvi wa samaki wale na aina yake ni tofauti sana na samaki wengine. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa tamko ili wavuvi wa ngere kwenye Visiwa vya Ukerewe na maeneo mengine wasibughudhiwe ili wafanye shughuli zao za uvuvi wa samaki hawa bila shida yoyote. Nashukuru sana?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mkundi na timu ya Waheshimiwa Wabunge katika eneo la Ziwa Victoria kwa namna ambavyo mara kadhaa wamekuwa wakisimamia maslahi mapana ya wapigakura wa eneo hili ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi yetu kupitia sekta hii ya uvuvi. Sasa swali la kwanza la Mheshimiwa Mkundi linahusu juu ya ya Serikali kuwa tayari kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Victoria kama ambavyo tunafanya utafiti kwenye maji ya bahari ili kuweza kuruhusu nyavu ya chini ya milimita nane kuweza kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa upande wa bahari bahari zilizokuwa zikitumika ni milimita 10 na zimekubalika kuonekana na maoni ya wadau kuwa milimita 10 zimeshindwa kukamata dagaa na ndio maana Serikali tukaielekeza Taasisi yetu ya Utafiti (TAFIRI) kufanya utafiti na kujiridhisha ya kwamba tufanye mabadiliko ya kanuni kwa haraka ili ikiwezekana tuweze kutumia nyavu za milimita nane ili kuweza kuwabnufaisha wavuvi wa upande wa bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai hii ya kutaka tutumie njia hiyo ya utafiti kwa upande wa Ziwa Victoria, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mkundi na Waheshimiwa Wabunge wote wavuvi wa kutoka Ziwa Victoria tunaichukua rai hiyo na tutawaelekeza TAFIRI waweze kufanya utafiti na kuweza kujiridhisha bila ya kuathiri sekta hii ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mkundi linahusu uvuvi wa samaki aina ya gogogo, ngere na ningu. Samaki hawa ni samaki wenye kupendwa sana katika eneo la Ziwa Victoria naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika mabadiliko ya kanuni tunayoyafanya hivi sasa tumezingatia kwamba tufanye makubaliano ya kuweza kupitisha kanuni rasmi sasa ya kuweza kuvua na kutumia rasilimali hii ya samaki hawa aina ya gogogo, ningu na ngere ambao wameonekana katika kanuni zilizopita kuwa hawakutajwa moja kwa moja. Naomba niwahakikishie wavuvi wote wa eneo la Ziwa Victoria Serikali inalifanyia kazi jambo hili na muda si mrefu watapata matokeo ili waweze ku-enjoy na kufurahia rasilimali za Taifa lao.