Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:- Barabara za Makete Njombe na Itone - Ludewa zipo katika ujenzi lakini ujenzi huo unakwenda pole pole sana:- Je, ni lini ujenzi wa barabara hizo utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hadi sasa amefikia asilimia 25.2 barabara inayokwenda Njombe - Makete na asilimia 20 barabara ya Itone – Ludewa: Je, kama sasa hivi ni asilimia 25 na mwakani mwezi wa kwanza iwe imekamilika, ni muujiza gani utatendeka hapo kuikamilisha kwa miezi nane tu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hali ya barabara za Njombe Mjini na Vijijini ni mbaya sana kwa kuwa mvua sasa hivi zinaendelea kunyesha. Kuna hali mbaya sana kwenye zile barabara na watu sasa hivi wamesimamisha shughuli, hawawezi tena kusafirisha bidhaa au mazao: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inakarabati barabara hizi kwa haraka iwezekanavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba tuko asilimia hizo 25.2 na asilimia 20 kwa eneo la Itone – Ludewa, lakini labda nilifahamishe tu Bunge lako kwamba Mkoa wa Njombe hali ya jiografia yake ni maalum sana, ni special. Udongo wa Njombe siyo mchezo, kwa hiyo, hata kufikia asilimia hizi ilitakiwa Mheshimiwa Mbunge aipongeze Serikali. Ndiyo unaona kwamba barabara hii ambayo tunaijenga Lusitu - Mawengu ni barabara chache sana tumeweza kujenga kwa kiwango cha zege.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana hata na udongo wake tuliotumia kwa ujenzi, ulikuwa unatoka zaidi ya kilometa 200, kwa sababu udongo wa Njombe uko maalum kidogo. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango kazi ambao sisi kama Serikali tunausimamia, tutahakikisha kwamba kila wakati tunakwenda nao ili kama kutatokea zile natural calamity kama mvua kuwa nyingi, kama maporomoko katika maeneo haya, hata juzi tu barabara hii ilijifunga kwa sababu udongo wake unaporomoka sana. Kwa hiyo, nasi tunachukua hatua kila wakati ili kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho, ujenzi unaendelea, tukamilishe mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ule mpango kazi yaani action plan tutaendelea kuisimamia ili kuona kama kutakuwa na matatizo makubwa ya hali ya hewa tuangalie alternative ya kufanya barabara hii ikamilike na barabara hii wananchi wa Njombe na Watanzania wanaitumia. Kwa hiyo, miujiza ni ile ya Mungu kwamba tunasimamia vizuri na mvua ziwe nzuri, tuombe Mungu pamoja ili tukamilishe barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu (b), amesema barabara za vijijini hali ni mbaya. Ni kweli kama nilivyosema, hali ya jiografia ni mbaya, lakini sisi tumejipanga vizuri ndiyo mana utaoa kwamba tunao mpango kama tukipata fedha tutaanza kutengeneza hii barabara ya kipande cha kutoka Kibena kwenda Lupembe kwenye mpango wa manunuzi tunaoendelea nao, kilometa 50, tuanze kupunguza na kuwafanya wananchi wa maeneo ya Njombe waweze kwenda Morogoro kupitia Madeke na Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, yale maeneo ambayo yako korofi sana, tunaendelea kujenga barabara za zege kwa hiyo, zipo kilometa 126, ukitoka Lupembe pale ziko kilometa ambazo tunaendelea kuziunganisha na wananchi sasa wana-enjoy magari yanatoka Mlimba yanakuja Njombe. Kwa hiyo, ni hatua za Serikali kuwajali wananchi wa Njombe kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge, hata hii barabara tunayozungumza ya kutoka Mawengi – Lusitu, sehemu ya Itoni kwenda Lusitu na yenyewe tunaitazama kwa sababu ni muhimu tuwaunganishe vizuri. Pia tunatengeneza daraja kule Mto Ruhuhu ili wananchi hawa wa Njombe tuwaunganishe vizuri na wenzao wa Manda kule Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa ufupi kwamba tumejipanga vizuri, Njombe iko so special lakini nasi kama Serikali tuko special kwa ajili ya Njombe ili wananchi wapate huduma vizuri.