Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:- Halmshauri ya Longido inatakiwa kuwa na watumishi 1,660 wa kada mbalimbali lakini kwa sasa wapo 1atumishi 1,117 tu, hivyo, kuna upungufu wa watumishi 543 na wengi wao ni Watendaji wa Vijiji, Kata, Madereva na Makatibu Muhtasi:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vibali vya kuajiri watumishi wanaohitajika ili kuondoa upungufu uliopo? (b) Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuwathibitisha maafisa wanaokaimu wenye sifa za kuajiriwa?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamuuliza maswali ya nyongeza, nichukue fursa hii kumpongeza Naibu Waziri wa Utawala Bora na Utumishi japokuwa ni muda mfupi tu tangu apewe dhamana ya kusimamia nafasi hiyo utendaji wake unaonekana na kasi yake nafikiri ni sehemu ya kasi anayohitaji Rais wa nchi kuona katika utendaji wa Mawaziri wetu. Hongera sana mama, nakuomba uendelee kukaza buti umsaidie Rais kazi aliyokupa dhamana ya kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, swali langu la kwanza, kwa kuwa katika Wilaya ya Longido lenye jumla ya vijiji 49, kuna vijiji 22 ambavyo mpaka sasa hivi havina Watendaji wa Kijiji walioajiriwa, wako wanaokaimu tena wengine wamekaimu kwa miaka mingi. Ni lini sasa Serikali inakwenda kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Longido kibali cha kuajiri Watendaji hao ili kuziba pengo lililopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kupata majibu kwamba kwa kuwa katika baadhi ya zahanati tulizonazo katika Wilaya yangu ya Longido na vituo vya afya na kuna vingine viko mbioni kukamilishwa kama kile cha Kimokorwa, Engarenaibo na kadhalika ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi na naamini Serikali mwaka huu watatupatia bajeti ya kuvimalizia. Pia Hospitali ya Wilaya ambayo nayo imeanza kujengwa na inakwenda kasi na hata Siha nimeona Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa jumba la ghorofa linakalibia kukamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi watapatikana ili facility hizi ziweze kutoa huduma shahiki kwa Watanzania? Ahsante.

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza yote kwa pamoja ya Mheshimiwa Mbunge Kiruswa wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana kwa pongezi, nazipokea, aendelee tu kuniombea kwa Mungu ili nisiwaangushe Watanzania wote na Mheshimiwa Rais mwenyewe. Pia na yeye binafsi nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye Jimbo lake la Longido hususani katika kufuatilia huduma zinazotolewa na watumishi wa umma kwa wapiga kura wake wa Jimbo la Longido.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu tu kwa ufupi na kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi zote za kukaimu; kwanza kukaimu ni nafasi ya muda, wala siyo ya kuthibitishwa. Naomba niwaeleze Watanzania wote kwa faida ya wengine, kwa sababu kuna wengine huwa wanafikiri kwamba ukipewa nafasi ya kukaimu, basi ndiyo leeway yako ya kuthibitishwa, hapana. Kukaimu unakaimu kwa muda na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu kwa sababu watu wamekuwa wakikaimishwa kienyeji bila kufuata utaratibu. Utaratibu ni kwamba unapotaka kumkaimisha kiongozi yeyote yule ambaye ameshafikia katika ile level ambayo tunaita superlative substansive post (nafasi ya uongozi) basi unatakiwa kupata kibali kutoka utumishi. Utumishi wakupatie kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwaka 2018 mwezi Septemba, Serikali yetu imetoa waraka kwamba nafasi zote zile za kukaimu zisizidi miezi sita. Unapotaka yule Afisa aendelee kukaimu, basi unatakiwa utoe sababu nyingine wewe kama Mwajiri kwa nini unataka aendelee kukaimu? Hiyo yote ni katika lengo la kuboresha ili viongozi wetu wasiwe wanakaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, kwenye jibu langu la msingi nimesema katika Jimbo lake la Longido tumetoa vibali na nafasi za ajira 177. Katika hizo 177, 65 zinakwenda katika Sekta ya Afya, 69 zinakwenda katika Sekta ya Elimu na zinazobaki nyingine zote zinakwenda katika kada nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika zile kada nyingine ambazo ni za kimuundo, zenyewe hazihitaji kukaimishwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mwaka huu wa Fedha 2018/2019, hizi nafasi 177 tutakuwa tumeshazijaza katika Wilaya ya Longido hususan Jimbo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwanjelwa kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze jibu kwenye swali linalohusiana na Watendaji wa Serikali za Mitaa. Hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge wa Longido ni kweli, lakini naomba niseme tu kwamba kupata Watendaji kwenye ngazi za Halmashauri na huu ni mwaka wa bajeti kwenye Bunge hili Tukufu, tunatarajia Wakurugenzi ambao ndio waajiri wa watu hawa, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mitaa watakuwa wameingiza kwenye bajeti zao ili tupitishe na waweze kupata ajira. Kwa hiyo, Wakurugenzi wanapaswa kujua upungufu wa maeneo yao ya kiutendaji, kama wakiwasiliana na Ofisi ya TAMISEMI kwamba hawa watu wanafanya kazi kubwa sana waweze kusaidiwa utendaji katika ngazi ya chini. Ahsante.