Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Handeni ambao wanakosa ardhi ya kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu ya kumilikiwa na wachache?

Supplementary Question 1

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Wilaya ya Handeni ni Wilaya kubwa sana lakini kwa bahati mbaya hawana Baraza la Ardhi kiasi kwamba yanapotokea matatizo yanayohusu ardhi inawabidi wananchi kusafiri mpaka Wilaya ya Korogwe:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi hawa Baraza la Ardhi?

Swali la pili; kumekuwa na migogoro ya muda mrefu katika Vijiji vya Sezakofi Kata ya Ndolo, Wilaya ya Handeni na Kata ya Kwagunda Wilaya ya Korogwe:-

Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atakwenda kuwaona wananchi hawa ili kusikiliza kero zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Sonia ameuliza ni lini tutaweka Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Handeni, kwa sababu sasa hivi wanakwenda Korogwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu nimfahamishe kwamba ni dhamira njema ya Serikali kuhakikisha kwamba inakuwa na Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya. Mpaka sasa tuliyonayo kisheria ni mabaraza 97 ambapo 53 yanafanya kazi na 44 hajaweza kuanza kufanya kazi. Tatizo kubwa lililopo katika uanzishwaji wa mabaraza, jambo la kwanza ni ile rasilimali watu wa kuweza kuhudumia mabaraza hayo lakini pia na maeneo au majengo kwa ajili ya kufanyia shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, pia tunapeleka baraza pale ambapo pengine pana mashauri mengi kiasi kwamba panahitaji nguvu ya ziada. Ni hivi karibuni tu tumeongeza mabaraza mengine likiwemo la Mbulu na maeneo mengine kwa sababu tu tayari tulishapata nafasi ya ofisi katika eneo lile na sisi jukumu letu kama Wizara ni kupeleka watumishi pamoja na samani za ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaangalia tawimu zilizopo kwa Handeni kama kweli ni nyingi kiasi cha kutaka kuwa na baraza, basi nitawaomba uongozi wa pale watuandalie eneo ambalo litakuwa ni ofisi linalokidhi vigezo vya kuwa Baraza la Wilaya. Vinginevyo nitawaomba waendelee kutumia Baraza la Korogwe kwa sababu lipo karibu na bado hawana mashauri mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ameuliza ni lini nitakwenda katika eneo la Handeni kwenye Kata ya Sasako na Kwagunda kwa ajili ya kutatua migogoro. Naomba nimthibitishie tu kwamba ni dhamira njema ya Wizara kuhakikisha kwamba tunafika maeneo yote yenye migogoro lakini kabla hatujafika, uongozi uliopo katika maeneo yale unafanya kazi nzuri sana ya kuweza kutatua migogoro. Pale ambapo inashindikana na uongozi uliopo pale, basi Wizara ipo tayari kufika. Kwa kesi yake huyu, basi tutaangalia uwezekano wa kuweza kwenda kutatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mbunge wa eneo lile, Mheshimiwa Mboni, amekuwa akiulizia pamoja na jirani yake Mheshimiwa Kigoda, nikawaambia tutafika pale. Nilikuwepo mwaka 2016 lakini nitatafuta muda tena kama bado kuna kero, tutaenda kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nataka kutoa nyongeza nimfahamishe Mheshimiwa Sonia kwamba takwimu zinaonyesha kwamba mashauri mengi ya ardhi yalikuwa yanatoka Wilaya ya Lushoto ndani ya Mkoa wa Tanga. Kwa hiyo, Serikali hivi sasa imefanya jitihada ya kuongeza Baraza jipya la Lushoto ili kupunguza load ya mashauri ndani ya Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa tumeanzisha baraza, ukiacha Korogwe ambao walikuwa wanahudumia mpaka Lushoto, sasa Lushoto wanajitegemea. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo maana yake hata Handeni sasa mtapata huduma nafuu zaidi kwa sababu nusu ya matatizo ya kero ya ardhi ya Tanga sasa yamepatiwa ufumbuzi kwa kumpeleka Mwenyekiti mpya Wilaya ya Lushoto.

Name

Mboni Mohamed Mhita

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Handeni Vijijini

Primary Question

MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Handeni ambao wanakosa ardhi ya kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu ya kumilikiwa na wachache?

Supplementary Question 2

MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Naomba nitumie fursa hii kwanza kuipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua kubwa ambayo Wizara imekuwa ikiendelea kufanya hasa katika zoezi zima la kutoa notice kwa wakulima wakubwa wenye kuhodhi maeneo makubwa. Nami ni shahidi kabisa kwa Jimbo la Handeni Vijijini, zoezi hili limekuwa linaendelea kwa kasi na limepelekea wananchi wa Jimbo la Handeni sasa kujikita sana kwenye kilimo cha muhogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe tu ushuhuda hasa kwenye Kata ya Kabuku na Mkata sasa hivi zoezi hilo linaendelea na Halmashauri imekuwa ikipambana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri, kasi hii iweze kuendelea kwa sababu Handeni, hususan Jimbo la Handeni Vijijini tuna maeneo makubwa sana japokuwa mpaka sasa kwa kusema kweli nitoe tu ushuhuda kwamba hakuna conflict ya maeneo. Wananchi wameendelea kujitoa sana na kilimo cha muhogo na mpaka sasa hivi ni mashahidi kwamba Handeni tunaongoza kwenye kilimo cha muhogo na tunapata viwanda ambacho Serikali kupitia Balozi wetu wa nchini China wametuletea kiwanda cha mihogo ambacho tunategemea hivi karibuni kitaanza kujengwa.

MWENYEKITI: Haya ahsante.

MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; naomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kutuambia zoezi hili litaendelea mpaka lini kwa sababu wananchi wa Jimbo la Handeni wanaendelea kuwa na chachu kubwa sana ya kuweza kupata. Nashukuru.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mboni Mhita, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze na nimshukuru kwa kupongeza Serikali, lakini niseme tu kwamba zoezi hilo aliloliuliza nadhani sio kwa Handeni peke yake, zoezi hili linatakiwa kufanyika nchi nzima. Zoezi hili linatakiwa kufanywa na halmashauri husika zenyewe, wao ndio wenye maeneo, ndio wanajua nani kaendeleza, nani hajaendeleza. Kwa hiyo nitoe rai kwa halmashauri zote; jukumu lenu ni kuhakikisha mnafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mashamba ya wawekezaji ambao hawajaweza kuyaendeleza. Wakituletea taarifa Mheshimiwa Waziri atamshauri Mheshimiwa Rais kuyafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunapokea kutoka kwao, Wizara sio inayoanzisha ufutwaji wa mashamba au ukaguzi unafanywa na halmashauri husika. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, jukumu hili ni la halmashauri, naomba walitekeleze na sisi kama Wizara tuko tayari kuwasaidia kumshauri Mheshimiwa Rais.

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Handeni ambao wanakosa ardhi ya kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu ya kumilikiwa na wachache?

Supplementary Question 3

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina swali dogo la nyongeza; tatizo la Baraza la Ardhi kwa Mkoa wa Kigoma ni tatizo sugu na mashauri mengi ya ardhi katika Mkoa wa Kigoma yapo katika Wilaya ya Kasulu, wameshafanya utafiti wa kuanzisha baraza pale lakini huu ni mwaka na nusu sasa. Je, ni lini wanatuanzishia Baraza la Ardhi Kasulu ili kupunguza matatizo ya ardhi na watu wasiende Kigoma na wengine kutoka Kibondo kwenda Kigoma?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika mabaraza mapya ambayo yameanzishwa nadhani na Kasulu limo kama kumbukumbu zangu ziko vizuri. Kwa hiyo nasema tutafika tuweze kuona eneo ambalo limeandaliwa kwa ajili ya baraza kwa sababu katika yale yaliyoongezeka nadhani na Kasulu imo. Ahsante.