Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:- Je, ni lini wananchi wanaodai fidia ya maeneo yao yaliyopitiwa na mradi wa KV 400 katika Jimbo la Babati Mjini watalipwa.

Supplementary Question 1

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mimi nina mambo mawili, la kwanza ni ombi, la pili ni swali.

Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza naipongeza Serikali. Hivi ninavyoongea leo, tangu siku ya Ijumaa na leo asubuhi Jumatatu watu wa KV 400 wako Babati eneo la Singu wakilipa wananchi fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu kwa Serikali, kwa kuwa kuna sintofahamu kati ya wananchi na Mwekezaji katika shamba la Singu, wananchi walikuwepo tangu miaka ya 1970, mwekezaji amepewa hati mwaka 2011 na wananchi wanalipwa asilimia 34 leo ya ardhi. Hebu niiombe Wizara ya Ardhi, ilitazame hili jambo upya, waone kati ya wananchi na mwekezaji, ni nani mvamizi, ili haki itendeke wale wananchi walipwe asilimia 100 ya ardhi.

Swali sasa kwa Wizara ya Nishati. Mheshimiwa Naibu Waziri, siyo wananchi wote wanaolipwa, leo wanalipwa tu Sigino pale, lakini mtaa wa Sawe, Maisaka Kati, Kijiji cha Kiongozi na Malangi, wao cheki zao hazijaandaliwa mpaka sasa. Naomba nifahamu, ni lini Wizara ya Fedha na Mipango nao watamaliza kukamilisha cheki hizi ili na hao wananchi waweze kulipwa? Maana mazao yao yameshafyekwa na mradi unaendelea. Ni lini cheki zao zitafika?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo umesema, swali la kwanza ni ombi; lakini kabla sijaendelea, naomba nitoe pole kwa wakazi wa Mkoa wa Manyara, kufuatia kifo cha Meneja wa TANESCO wa Mkoa huo wa Manyara, pamoja na Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Mbulu ambao walifariki siku za hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, napenda nijibu hili swali la pili, ambalo Mheshimiwa Pauline Gekul ameuliza Mitaa ya Sawe, Mwaisaka Kati, Kiongozi, lini watalipwa fidia zao? Kwa kuwa Wizara ya Fedha ilifanya uhakiki na kukabainika baadhi ya changamoto na ikapelekea sasa kupeleka watathmini wengine ambao walifanya mapitio; hivi ninavyosema, jedwali jipya ambalo linawasilishwa kwa Ofisi ya Mtathimini Mkuu wa Serikali, limeshafika Dodoma na Mtathimini Mkuu wa Serikali yuko katika hatua za mwisho za kusaini na kisha malipo yataandaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa hili suala mara kwa mara, pamoja na wananchi wake. Nimwahidi tu kwamba, hili suala kwa kweli kwa kuwa amesema na yeye na sisi tumepokea pongezi, malipo yameanza kwa wakazi wa maeneo hayo ya Sawe, Mwaisaka Kati, Kiongozi, kwamba malipo yatafanyika siyo muda mrefu kuanzia sasa kama ambavyo jibu letu la msingi limesema. Ahsante.

Name

Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:- Je, ni lini wananchi wanaodai fidia ya maeneo yao yaliyopitiwa na mradi wa KV 400 katika Jimbo la Babati Mjini watalipwa.

Supplementary Question 2

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la fidia lililopo Babati linafanana kabisa na tatizo la fidia lililopo katika mradi wa umeme wa Rusumo Wilaya ya Ngara. Je, ni lini wananchi wa Kata ya Mlukulazo na Mtobee watalipwa fidia kwa maeneo yao yaliyoathiriwa na mradi wa Rusumo?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver la masuala ya fidia katika mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Rusumo la megawati 80 pamoja na njia yake ya Msongo wa KV 220 kutoka Rusumo - Nyakanazi. Kwanza Mheshimiwa Mbunge Oliver nimpongeze kwa kufuatilia suala hili la malipo ya fidia; lakini kwa kuwa mradi umeanza na fidia ililipwa pengine wapo wananchi ambao wana malalamiko au bado hawajalipwa, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, baada ya hapa tu nitalifuatilia kuona wakazi wa Kata ya Mlukulazo na Kata nyingine ambayo ametaja kwamba wanalipwa stahiki zao kwa sababu mradi ule unaendelea mpaka sasa ambao una manufaa makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.