Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, Serikali iko tayari kubadilisha sheria/kanuni ili kuruhusu mazao ya misitu kusafishwa usiku na mchana (saa 24)?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kabla ya maswali haya mawili ya nyongeza naomba kuitahadharisha Serikali katika jibu la msingi Serikali inasema kwamba watatoa vibali.

Katika suala la vibali bila shaka litaleta mazingira ya rushwa ili watu waweze kupata hivyo vibali na bila shaka litaongeza shida na watu wetu wataendelea kupata tabu sana.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza la kwanza, ikiwa katika majibu ya msingi ya Serikali inakiri kwamba hali imeimarika ya watumishi na mambo ya udhibiti na mambo ya ukaguzi. Je, sasa Serikali haioni ikiwa hali imeimarika ni wakati muafaka wa kuondoa zuio hili ili kusudi mazao ya misitu yapate kusafirishwa muda wowote kadri mtu anavyotaka ku- speed up uchumi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu wakati mwingine Serikali ina shaka sana na mbao pori na bahati nzuri Mheshimiwa Spika wewe ni mhifadhi. Je, Serikali iko tayari kuturuhusu sisi ambao mbao hizi, nguzo, mirunda zinatokana na miti ambayo tumepanda sisi wenyewe na siyo mbao pori. Je, Serikali iko specifically tayari kuruhusu kwa mbao ambazo zinatokana na miti ya kupandwa ziruhusiwe kusafirishwa muda wowote ambao mwananchi au mfanyabiashara anaona kwake ni muafaka ili ku-speed up uchumi kwa sababu Serikali iko kazini 24/7 masaa 24 siku saba, hakuna mahali Serikali imelala na inafanya ikaguzi kuna vituo, magari ya patrol. Je, Serikali iko tayari hasa kwa miti ambayo sisi watu wa Mafinga, Mufindi, Iringa, Njombe, Ruvuma tunapanda kwa nguvu zetu kuruhusu?

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Cosato Chumi kwamba tukiweka mazingira magumu ya upatikanaji wa vibali tutasababisha vibali hivi kutolewa kwa upendeleo na pengine kutasababisha kuchochea rushwa nakubaliana naye. Kutokana na sababu hiyo ndio maana tumesema kwa sasa tumefikia mahali huduma zimeimarika na tutaondoa zuio la usafirishaji wa mazao ya misitu kutokana na misitu ya kupandwa ambayo ilikuwa inasafirishwa mchana peke yake sasa kuanza kusafirishwa kwa masaa 24. Nafikiri hilo tayari katika majibu yangu ya msingi nilisema na tuko kwenye hatua za mwisho za kuondoa zuio hilo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tutaendelea kuwa na zuio kwenye mbao za misitu ya pori na hii ni kwa sababu ya kulinda kwanza misitu yenyewe ambayo inaelekea kutoweka, lakini pili kuendelea kuisimamia vizuri ili kupunguza udanganyifu. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ruhusa ya usafirishaji wa misitu ya kupanda ambayo nimeizungumzia ikiwa ni pamoja na mirunda na mazao yake tutaitoa hivi karibuni na hapatakuwa na masharti kwa mtu ambaye amekamilisha vibali.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na yenye kujitosheleza ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nikupe comfort kwamba suala hili tumeshaanza kulifanyia kazi hata kabla ya kupokea swali la kutoka kwa Mheshimiwa Chumi na tupo katika hatua za mwisho mwisho za kuweka utaratibu kwa ajili ya kufungua usafirishaji usiku wa mbao ambazo ni za kupanda.

Mimi binafsi sio muumini sana wa kuzuia watu wasifanye kazi usiku mara mabasi hayasafiri usiku, mara malori hayasafiri usiku, mbao hazisafiri usiku, tunachelewesha ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mtazamo wangu ni kwamba ili kutia chachu ya ukuaji wa uchumi watu ni lazima wafanye kazi mchana na usiku na ndio maana nimetoa agizo ndani ya Wizara kwamba walete ushauri wa kitaalam wa namna ambavyo tutaweka control ili kudhibiti uhalifu na vitu vingine lakini watu waruhusiwe kusafirisha mazao yao usiku.