Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Primary Question

MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Kulikuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo; wananchi wa vijiji hivyo walienda mahakamani na wakaishinda TANAPA kwa sababu mipaka iliyokuwa iwewekwa na TANAPA haikuwa shirikishi na haikufuata GN iliyoanzisha SENAPA:- (a) Je, ni lini Serikali itapitia upya mipaka hiyo kwa kushirikisha vijiji husika na kuzingatia GN iliyoanzisha SENAPA? (b) GN iliyoanzisha IKorongo Game Reserve inatofautiana na mipaka iliyowekwa; je, ni lini marekebisho yatafanyika ili iendane na GN?

Supplementary Question 1

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Vijiji vyenye mgogoro wa mipaka na Hifadhi ya Serengeti ni vijiji vinane, Kijiji cha Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisalala na Bonchugu. Ukiona wananchi wa vijijini wameungana, wameenda mahakamani, wameishinda Serikali, halafu Serikali imekata rufaa ni kama kuwaonea na wananchi hawana shida na mambo ya rufaa.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Serengeti imeanzishwa kwa GN namba 235 ya mwaka 1968 na ikatengenezewa ramani iliyosajiliwa kwa registration namba 14154. Ramani hii imefichwa, imeanza kutengenezwa ramani nyingine na ndio kisa cha wananchi kushinda mahakamani. Sasa tunataka kujua kwa nini Serikali haitaki kwenda kukaa na wananchi wa vijiji hivi ili kukubaliana mpaka, sio kupoteza muda kukaa huko mahakamani na wananchi wanaumia. Kwa hiyo ni lini Wizara na Wizara ya Ardhi wataenda kukaa na wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ni kweli imekiri kwenye barua kwamba ilifanya makosa kwenye kutekeleza mipaka kwenye GN iliyoanzisha Pori la Ikorongo, wamekiri na wanahitaji utaratibu tu wa kwenda kurekebisha ile mipaka. Kwa nini Wizara pamoja na Wizara ya Ardhi wasiende kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya kurekebisha ile mipaka?

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haiwezi kuwa na lengo la kuonea wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema, lakini taasisi hizi zilipokuwa zinapitia mipaka na baada ya migogoro hii kuwepo na baada ya wananchi kushinda kwenye kesi yao ambayo walikuwa wamefungua, Taasisi kwa sababu ilikuwa inafahamu mipaka yake ya awali iliamini kwamba ikikata rufaa inaweza ikabadilisha matokeo. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi sisi Serikali baada ya kesi hii kwenye Mahakama ya Rufaa kuamuliwa tutatumia hukumu hiyo kuweka mipaka ambayo itamaliza mgogoro huu na kama mipaka hiyo itakuwa ni hii ya sasa ambayo vijiji vinatambua, hatuna pingamizi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi tutakwenda kupitia upya hii mipaka ya Ikorongo na kuweka alama kwa kutumia Wizara ya Ardhi pamoja na ushirikiano na Wizara yetu ili kumaliza mgogoro huu kwenye suala lake la pili.