Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Primary Question

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:- Kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya Mamlaka za Maji Safi katika Halmashauri mbalimbali kwa kuwapatia wananchi bili kubwa za maji ambazo haziendani na uhalisia:- Je, ni lini Serikali itaanzisha utaratibu wa kulipia maji kadri utumiavyo katika utoaji wa huduma hiyo kama ilivyo kwenye umeme?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri nakushukuru sana kwa majibu mazuri. Kwa kweli hicho ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi kuhusu bili na kuhusu upatikanaji wa hizi pre-paid meters.

Mheshimiwa Spika, katika jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imeagiza Mamlaka zote nchini kuendelea kuwafungia wananchi; swali langu ni kwamba: Je, ni lini sasa wamewaagiza muda wa kumaliza kufunga hizi meters? Maana isije ikachukua muda mrefu, tuweze kuwapunguzia adha hii ya bili kubwa na wananchi waweze kupata maji kwa bili ambayo ni ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, hii ni changamoto, lakini sisi kama Wizara tumeliona. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwatetea wananchi wake wa Morogoro pamoja na Watanzania kwa ujumla kutokana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza tumewaita Wakurugenzi wote katika Wizara yetu kwa maana ya Mamlaka za Maji na Mheshimiwa Waziri akawapa agizo hili kutokana na changamoto hii. Kikubwa, sisi katika kuhakikisha tunaongeza utendaji, tumewasainisha mikataba (performance agreement) kwa maana ya utendaji wao. Huwezi ukawa Mkurugenzi wa Maji halafu kumekuwa na changamoto katika suala zima la upatikanaji wa maji. Kwa hiyo, ninachotaka nimhakikishie, sisi kama viongozi wa Wizara tutawapima kwa yale maagizo tuliyowapa kuhakikisha wanatekeleza kwa wakati ili kuweza kuondoa changamoto hizi za bei pamoja na maeneo mengine ambayo hayajafikiwa na usambazaji wa maji.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.