Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Neema William Mgaya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- MSD kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa za kuongeza damu kwa mama mjamzito na dawa za usingizi:- Je, ni lini changamoto hiyo itatatuliwa?
Supplementary Question 1
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikiri kwamba sisi watu wa Mkoa wa Njombe hospitali zetu na vituo vyetu vya afya tunapata pesa za dawa zaidi ya asilimia 90, lakini bado Mheshimiwa Naibu Waziri kuna changamoto. Tuna changamoto ya dawa za afya ya akili pamoja na chanjo ya kichaa cha mbwa ambazo inatulazimu vifaa vya afya kwenda kununua kwa wa zabuni kwa bei kubwa sana. Sasa je, ni lini MSD itatatua changamoto hii kuhakikisha kwamba, inapeleka dawa za afya ya akili na chanjo ya kichaa cha mbwa katika vituo vya afya na hospitali za Mkoa wa Njombe?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, pesa za Basket Fund zimekuwa zikichelewa sana katika vituo vyetu vya afya na hospitali zetu za Wilaya ndani ya Mkoa wa Njombe. Hivi sasa ninavyozungumza Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, Hospitali ya Wilaya ya Makete, wamepata pesa za Basket Fund kwa quarter ya kwanza tu ilihali sasa hivi tuko quarter ya tatu. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa hizi za Basket Fund kwa wakati ili hospitali hizi ziweze kununua dawa kwa sababu bila kuwa na pesa hata waki-place order kule MSD, MSD hawakubali kuwapatia dawa?
Name
Dr. Faustine Engelbert Ndugulile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mgaya kwa kuwa mfuatiliaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kule Njombe katika kuwahudumia akinamama na watoto. Sasa naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi Serikali ni utaratibu unaitwa pull system, hapo awali tulikuwa tunapeleka dawa pasipo kuzingatia mahitaji na uhalisia ambao ulikuwepo katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Sasa hivi utaratibu ni kwamba hospitali zinaagiza kulingana na mahitaji yake na nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, chanjo tunazo zote asilimia mia moja na hizi tunazisambaza kulingana na mahitaji ya mikoa.
Mheshimiwa Spika, la pili, chanjo za kichaa cha mbwa na dawa za afya ya akili; dawa hizi tunazo katika bohari yetu ya madawa na katika stoo zetu za kanda pale Iringa. Niombe tu Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuwaomba mamlaka kule kuagiza kwa sababu zile dawa zina mahitaji mahususi, huwezi ukazipeleka tu kwa sababu wagonjwa wa afya ya akili pamoja na wagonjwa ambao wameumwa na mbwa si wengi kiasi hicho. Hata hivyo, sisi kama Serikali kupitia bohari ya dawa, tunazo dawa hizo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli tunakiri kwamba pesa za Basket Fund zinakuwa zinachelewa na hii kwa sababu fedha hizi nazo zina mkono wa wafadhili, wanapochelewa kutufikishia na sisi mchakato mzima unachelewa kuzifikisha kule. Hata hivyo, niseme tu kwamba fedha za Basket siyo chanzo pekee cha fedha ambazo zinatumika katika dawa, tuna fedha za ruzuku za dawa ambazo tunazipeleka, tuna fedha papo kwa papo na tuna fedha za bima ya afya ambazo zote kwa kiasi kikubwa nazo zinapelekwa katika manunuzi ya dawa. Kwa hiyo kutokuwepo kwa pesa ya Basket Fund, siyo kigezo na wala siyo sababu ya kukosekana dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved