Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felister Aloyce Bura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuza:- Kituo cha Polisi Chipanga kilijengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka 18 iliyopita:- Je, ni lini kituo hicho kitafunguliwa na kutoa huduma kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo nyongeza. Tangu mwaka 2017 mwezi wa Pili, huu ni mwaka wa tatu jengo hili halijawahi kutumika baada ya kulikabidhi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Wananchi wanatoka kilometa 30 kufuata huduma Dodoma Mjini badala ya kwenda Bahi ambayo ndiyo Wilaya iliyopo Tarafa ya Chipanga. Wananchi wanateseka kwa sababu hawana mahali pa kupeleka wahalifu wanapokamatwa. Je, Serikali iko tayari sasa kufanya ukarabati kwa mwaka huu wa fedha katika jengo hili ambalo tulikabidhi litumike kama Kituo cha Polisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa aandamane pamoja nami baada ya Bunge hili twende akaongee na wananchi ambao wamekaa kwa muda mrefu wakisubiri jengo lile litumike kama Kituo cha Polisi?

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Bura kwa namna ambavyo anachapa kazi kwa umahiri na juhudi kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma. Ndiyo maana Mheshimiwa Bura namfananisha na kumlinganisha na mama mmoja kwenye Biblia naitwa Ester. Mama huyu akiwa bikira alipata kibali machoni pa Mfalme Ahasuero wa kule Shushani Ngomeni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bura amepata kibali kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika kuwafanyia kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, ni kweli kwamba Kituo hiki cha Polisi cha Chipanga kina matatizo ambayo tumeyafanyia tathmini. Namhakikishia Mheshimiwa Bura awe na amani, kwamba kituo hicho baada ya kufanya tathmini, tutatenga fedha kwa ajili ya kwenda kukikarabati ili kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Chipanga katika Wilaya ya Bahi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Felister Bura nikukuhakishie kwamba huko unakotaka twende labda wewe ndio umechelewa, mimi niko tayari hata leo hii ukitaka tutakwenda wote kule Bahi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe wito kwa Mabaraza ya Madiwani kote nchini kwamba katika Ilani hii ya CCM, Ibara ya 146 chama kimeelekeza Serikali zake mbili kwa maana ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu. Nawaomba Waheshimiwa Madiwani, kwenye makusanyo ya ndani watenge pia fedha kwa ajili ya kujenga Vituo vya Polisi pamoja na nyumba za askari ili tuweze kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora kwa wananchi hapa nchi. (Makofi)