Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA aliuliza:- Seikali ina mkakati gani wa kujenga Kiwanda cha Kusindika Nyanya katika maeneo ya Mto Ngarenanyuki?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Waziri. Pamoja na majibu yake mazuri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza ni kuhusiana na uhalisia na Mto Ngarenanyuki. Mto huu ni moja ya mito michache ambayo imetokea katika maeneo yaliyohifadhiwa, unatokea katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha, chanzo chake ni salama na unapitisha maji mengi ya kutosha na kutiririsha katika nyanda za chini ambapo unapotoka ndani ya hifadhi, kijiji cha kwanza unafikia Kijiji cha Ngarenanyuki yanatiririka mpaka Kijiji cha Ngabobo na zamani za kale yalikuwa yanatiririka mpaka Kijiji cha Jimbo langu la Longido cha Ngereani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba; kwa kuwa maji haya yalipoingia Kijiji cha Ngarenanyuki wananchi wakagundua kwamba ni maji safi ya kuoteshea nyanya; wamekatakata mto mifereji mashine za kunyonya maji mtoni mpaka mto ukakaushwa na maji hayatiririki tena kwenda kwenye vile vijiji vya kusini zaidi. Serikali ina mpango gani wa kusanifu miundombinu ya umwangiliaji wa kisasa itakayowezesha matumizi bora ya maji haya ili yaendelee kutiririka kufikia jamii zilizo chini zaidi kwenye nyanda za chini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa tunakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa maji haya kutosha wakulima wa nyanya waliopo Ngarenanyuki, Ngabobo Mpaka Ngereani kuwafikia wote kwa mtiririko wa asili. Serikali haioni kwamba ni bora sasa wajenge tanki kubwa la kuvuta maji Ngereani ili nao waendeleze kilimo cha umwangiliaji wa nyanya; hasa ukizingatia kwamba ni kilomita 10 mpaka 20 tu katikati Ngereani kutoka mtoni?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stephen Lemomo Kiruswa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake yote mawili yamegusa utaalam ambao upo ndani ya Serikali ingawa haupo ndani ya Wizara yangu. Ni jambo la msingi alilolizungumza, kwamba kila Mtanzania anawiwa na dhima ya kulinda rasilimali za maji na hasa hasa kwa sababu haya maji mazuri yametoka katika eneo limeifadhiwa yalikuwa yanatiririka vizuri kwenda kwenye vijiji. Sasa wananchi wameya-tap na kuyachota na kupeleka kwenye miradi ya umwagiliaji bila kuzingatia ushauri mzuri wa kitaalam wa kutumia maji kidogo na kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi natoa ushauri kwa Tume ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bonde washirikiane, kwa sababu hizi ni mamlaka za Serikali, waende katika eneo husika wakawaelimishe wananchi kuhusu kilimo bora cha umwangiliaji bila kuchukua maji mengi kutoka kwenye mto ule ili maji yale yaifadhiwe yaendelee kutumika vile vile kwa shughuli zingine na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu ujenzi wa tanki kubwa litatokana na ushauri ambao wataalam wataona kadri inayofaa katika kutumia maji ya Mto Ngarenanyuki. Ahsante sana.