Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:- Ardhi ni rasilimali ya msingi katika nchi yoyote duniani na tamaa ya kupora ardhi imesababisha migogoro na vita:- (a) Je, Serikali ilitenga bajeti kiasi gani kuanzia mwaka 2010 – 2015 kwa ajili ya kupima matumizi ya ardhi? (b) Je, kati ya kilometa za mrada 945,000 za Tanzania ni eneo kiasi gani limepimwa hadi Disemba 2015?

Supplementary Question 1

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ukiangalia bajeti ambayo imekuwa ikitengwa kila mara kwa ajili ya hii kazi ya kupima matumizi ya ardhi ni ndogo sana. Mpaka sasa miaka 57 ya uhuru tumepima asilimia 15 tu ya nchi ya Tanzania na migogoro bado ni mingi kila siku kukicha kuna migogoro. Je, Waziri atakubaliana nami kwamba, kwa style hii migogoro haitaisha na kwamba, nchi itakuwa haina amani na utulivu kwa sababu ya migogoro ya ardhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mikoa mingapi ambayo mpaka sasa hivi imeanzisha Benki za Ardhi ili kurahisisha uwekezaji na pia kuwawezesha wakulima wakubwa? Ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Nyongeza ya Mheshimiwa Ruth Mollel kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anasema bajeti ni ndogo kiasi kwamba, migogoro bado inaongezeka kuwa mingi na huenda pengine ikasababisha kutokuwa na amani. Katika jibu langu la msingi nimeonesha takwimu ikionesha bajeti ilianza kiasi gani na sasa iko kiasi gani. Ilianza na bilioni 1.5 lakini sasa hivi tumefikia bilioni 6. 3. Kwa hiyo, ni vitu ambavyo vinaongezeka mara kwa mara, lakini kama hiyo haitoshi Wizara yangu inalo jukumu la kuwezesha halmashauri katika kuwapa uwezo wa kuweza kusimamia masuala ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha kwamba, eneo lote linapimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii imekuwa ikifanyika na mpaka sasa tunapoongea jumla ya vijiji 1,880 vimekwishafanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na sasa hivi tunazo wilaya kama 40 ambazo mpango bado unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo ni kwamba, pale ambapo halmashauri zinawezeshwa tuna imani kwamba, zoezi la upimaji litaendelea na sio kusubiri Wizara kwa sababu, sheria yenyewe inatamka wazi kwamba, mamlaka za kupanga na kupima maeneo ni halmashauri zetu za wilaya na vijiji katika maeneo. Kwa hiyo, ni jukumu pia la halmashauri zetu na sisi pia tukiwa ni washiriki katika mabaraza yetu, basi tusimamie zoezi hilo ili kila halmashauri iweze kutekeleza wajibu wake ambao inapaswa kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kuainisha ni mikoa mingapi, naomba swali hili nisimjibu kwa sababu linahusu takwimu, pia niweze kuwa na uhakika ni kiasi gani, nisije nikampa jibu lisilo sahihi. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima kila kipande cha ardhi. Ndio maana mwaka huu tumeamua kuandaa mradi mkubwa ambao utatuwezesha katika miaka mitano hii tuwe tumekamilisha upimaji na upangaji, upangaji na upimaji kila kipande cha ardhi nchini. Kwa hiyo, pamoja na hiyo fedha ya bajeti ya Serikali ya kawaida tumeamua tukope kwa sababu, ina faida kubwa zaidi kwa kupanga na kupima nchi nzima kwa wakati mmoja kwa sababu, vilevile tunajua itatusaidia katika kupata mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwananchi akimiliki kwa hati, atalipa kodi kila mwaka, kwa maana hiyo kila mtu atafaidika na upangaji na upimaji. Kwa hiyo, pamoja na hiyo ya bajeti, lakini Serikali tumeamua kuanzisha huo mradi mkubwa wa kupanga na kupima kila kipande cha ardhi na mradi huo utaanza mwaka huu baada ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza majaribio wilaya tatu, Kamati yetu ilikwenda juzi kuangalia namna tunavyoweza kufanya. Wameridhika na taarifa imetolewa jana kwamba, jambo lile linawezekana tukiwa na uwezo wa kutosha. Kwa hiyo, kutokana na ule mfano tulioufanya katika Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro tunataka kuusambaza nchi nzima mijini na vijijini. Kwa hiyo, jambo hilo Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge tunalifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumefanya uwezeshaji mikoani kwa kununua vifaa, jambo moja linalowafanya Halmashauri washindwe kupima na kupanga ni vifaa. Serikali, kupitia Wizara yangu, tumeshanunua vifaa vya kutosha vya upimaji ambavyo kila halmashauri inayotaka kupanga na kupima maeneo waende kwenye kanda wakaazime bila kukodisha ili viwasaidie katika zoezi la upangaji na upimaji kwenye wilaya zao.