Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Sera ya Afya imebainisha makundi yenye msamaha wa matibabu ambayo ni wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea, watoto chini ya miaka 5, watoto wanaoishi na TB na UKIMWI:- Je, ni lini Serikali itaweka Watu wenye Ulemavu kuwa miongoni mwa watu wanaohitaji msamaha wa gharama za matibabu?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda Serikali isikwepe wajibu wake wa kuhudumia watu wasiojiweza. Natambua kabisa kuwa kuna walemavu wenye uwezo lakini watu wengi wenye ulemavu wana matatizo mengi; kuna wale ambao ni yatima, kuna wengine ambao wametelekezwa na kuna wengine ambao kaya zao ni maskini sana. Ni kwa nini Serikali isiwajibike kuwahudumia watu hawa wenye ulemavu hasa kwa kuwatambua na pili kuwapatia bima ya afya bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema wagonjwa kuna wagonjwa wengi sana wa msamaha ambao wako katika hospitali zetu. Sawa wako wagonjwa wengi lakini ni lini Serikali sasa itatekeleza wajibu wake wa kutoa ruzuku katika hospitali zetu za mikoa au hospitali zetu za rufaa kwa sababu hawa wagonjwa ambapo wengine ni watu wenye ulemavu, watoto umri chini ya miaka mitano na wazee wanakwenda katika hospitali hizi kutibiwa na hizi hospitali zinakuwa na watu wengi ambao wanatakiwa kupata vifaatiba na vitendanishi? Ni lini Serikali itatoa ruzuku katika hospitali zetu ili ziweze kujikimu na kutoa huduma bora? Ahsante (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kutoa huduma za afya na haijawahi kusitisha kutoa huduma ya afya kutokana na sababu eti kwamba mtu anashindwa kugharamia matibabu. Hilo lipo vizuri ndani ya Sera yetu ya Afya na kuna makundi ambayo tumeyaainisha katika sera ambapo watu wanapata matibabu bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la walemavu kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, si kila mlemavu hana uwezo wa kupata matibabu, nataka niweke msisitizo. Ndiyo maana nimesema katika Sera hii Mpya tutaweka utaratibu mzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya sasa kati ya asilimia 60 - 70 ya wagonjwa ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya wanapata matibabu bure. Sasa hivi tunataka tuweke mfumo mzuri na kuhuisha na mifumo mingine kama ile ya TASAF kuhakikisha kwamba tunawatambua tu wale ambao kweli hawana uwezo na wanahitaji kupata matibabu. Tutakapokuja na huu utaratibu wa bima ya afya kwa wananchi wote tutakuwa na kundi dogo sana ambalo limebaki ambalo litakuwa linagharamiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini Serikali haipeleki ruzuku. Nimthibitishie Mheshimiwa
Mbunge na bahati nzuri naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na analijua na hivi karibuni tumetoa taarifa ya utekelezaji ya nusu mwaka, Serikali inapelekea mishahara hatujashindwa kupeleka mishahara, dawa na hela ya uendeshaji. Hakuna hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo haijapata huduma zote hizo ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna vyanzo vingi vya mapato ndani ya hospitali. Pamoja na ruzuku ya Serikali tuna fedha za papo kwa papo, fedha za bima na nyingine zinapata basket fund. (Makofi)