Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Kuendesha bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyingine nchini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo vijana hao ili kuifanya kazi hiyo iwe rasmi na yenye kutambulika kama kazi nyingine zozote?

Supplementary Question 1

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kuwa bodaboda zimetoa ajira nyingi sana hapa nchini. Je, Serikali haioni sasa kuwa kuna haja kubwa ya kuwawezesha vijana hawa mikopo kwa wakati kuliko ilivyokuwa sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi wamejiunga na vikundi na hawajawahi kupata mikopo, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kuona vikundi vile vya vijana na kuwapatia mikopo ambayo hawajawahi kuiona wala kuisikia, hasa kwa vijana wa Wilaya ya Lushoto?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali la kwanza la uwezeshaji kwa wakati kwa vikundi hivi vya bodaboda. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi ni kwamba Serikali inachokifanya hivi sasa ni kushirikiana na Mamlaka za Halmashauri, Manispaa, Wilaya na Majiji ili kuona namna bora ya kusaidia uundwaji wa vikundi hivi kwa sababu ni ngumu sana kumwezesha bodaboda mmoja mmoja pasipo kukaa katika vikundi. Ndiyo maana sasa hivi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani tumeendelea kufanya maandalizi kuhakikisha kwamba vyama hivi vya bodaboda katika mikoa na katika ngazi ya Taifa vinasajiliwa ili tupate namna bora ya kuweza kuwahudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mikopo linategemea utayari wa wahusika kwa maana ya kuunda vikundi na kuunda katiba ili wawe tayari kwa ajili ya kukopeshwa. Nitoe rai kwa vikundi vyote vya bodaboda nchini ambavyo viko rasmi watumie fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali na taasisi mbalimbali za fedha, hasa ukiwemo Mfuko wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ambao umelenga katika kuwapatia maendeleo vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kuhusu vijana wa Kilindi. Nitoe tu rai kwanza kwa Waheshimiwa Wabunge wote, wale ambao wana vikundi vya vijana na wangependa kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, sharti moja kubwa ambalo lipo ni uanzishwaji wa SACCOS ya vijana katika halmashauri husika. Hivyo, nipo tayari kwenda Kilindi pamoja na Mheshimiwa Omari Shekilindi kwenda kuangalia vikundi vya vijana. Vilevile kama watakuwa wamekidhi mahitaji ya uwezeshaji wa Mfuko wa Vijana basi tupo tayari kuwawezesha vijana wa Kilindi ili nao waweze kunufaika na fursa zilizopo katika nchi yao.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Kuendesha bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyingine nchini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo vijana hao ili kuifanya kazi hiyo iwe rasmi na yenye kutambulika kama kazi nyingine zozote?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba SUMATRA imefanya maboresho na inatoa leseni kwa waendesha bodaboda, nataka kujua ni kwa nini kumekuwa na restriction kwa bodaboda kuingiza bodaboda zao katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini vilevile ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hairuhusiwi? Naomba majibu ya Serikali.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mkoa wa Dar es Salaam uongozi wa mkoa uliweka utaratibu wa namna vyombo hivi vya usafiri vitakavyoingia katikati ya mji kutokana na changamoto ambazo zilijitokeza awali likiwemo suala la msongamano pamoja na usalama. Tayari kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wameanza kuratibu zoezi hili katika umakini mkubwa ili kuona namna bora ambavyo wafanyabiashara hawa pia watafanya biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika maeneo mengine zipo sababu za kimsingi za kwa nini yametokea masuala hayo lakini kubwa limekuwa ni suala la kiusalama. Ndiyo maana Serikali hivi sasa imeanza kuyatambua maeneo rasmi ya maegesho na kuwapatia vitambulisho ili likitokea jambo lolote la kiusalama tuweze kujua ni wapi limetokea na tuweze ku-trace ili kuondokana na dhana hii kwamba boaboda ni wahalifu.