Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:- Wilaya ya Mbeya, Mkoa wa Mbeya na Wilaya za Ileje na Songwe Mkoa wa Songwe zinaunganishwa kwa barabara za vumbi kuanzia Mbalizi kuelekea Ilembo, Iwinji hadi Ileje na Mbalizi kuelekea Mshewe. (a) Je, ni lini Serikali itaunganisha barabara hizo kwa lami? (b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi waliopisha upanuzi wa barabara za Mbalizi, Mshewe, Mjele hadi Mkwajuni Songwe?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nashukuru pia kwa majibu ya Serikali hasa kwa kutambua kuwa hizi ni barabara muhimu za kimkakati na kwa umuhimu huo huo ilikuwa ni ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami, ambayo ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete na pia ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuwa hizi barabara zijengwe kwa lami. Kwa umuhimu huo huo katika Ziara ya Waziri pamoja na Naibu Waziri nao kwa wakati tofauti walitembelea hizi barabara na kuona umuhimu wake na sasa labda ningependa kama ilivyo kwenye swali langu la msingi, ni lini barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole itajengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa umuhimu huo huo ni lini barabara ya Itewe - Mlima Nyoka - Songwe ambayo ni by pass itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Njeza kwa kufuatilia maendeleo ya Jimbo lake hususan mambo ya miundombinu. Maana yake hii naiona ni style ya Mpwapwa hii ni Lubeleje style, maana kila ukikutana nae anazungumzia juu ya barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba barabara hii natambua kwamba ni ahadi ya Viongozi, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba barabara hii ya Mbalizi – Shigamba – Isongole iko kwenye mpango mkakati wa Wizara kwa ajili ya kuiboresha. Kwa hiyo pindi tukipata bajeti tutafanya usanifu wa barabara hii na kuanza kuijenga katika kiwango cha lami. Vilevile kuhusu barabara hii ya Uyole – Mlima Nyoka hadi Songwe ambayo ni by pass Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba usanifu ulifanyika na kupitia Jiji la Mbeya na anafahamu kwamba eneo hili ni la uzalishaji mkubwa, kuna pareto inazalishwa kwa wingi lakini kuna viazi vinazalishwa kwa wingi, kuna mazao ya mbao, hii ni barabara muhimu pia kuna mahindi yanazalishwa kwa mwaka mzima katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi leo mtaalam mwelekezi anakwenda kufanya mapitio ya barabara hii kwa sababu uko uelekeo sasa wa kupata fedha ya kuijenga barabara hii by pass muhimu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nitaendelea kuku- update, kukupa taarifa zaidi tuone namna tunavyokwenda, lakini niseme tu kwa wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba tumejipanga vizuri sasa kuanza kuijenga hii by pass kwa ajili ya huduma muhimu katika eneo hili.