Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Uvuvi haramu bado unaendelea licha ya adhabu kubwa inayotolewa kwa watu wamaojihusisha nao. (a) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwasaidia wananchi wake fursa zilizopo badala ya kutoa adhabu kali zinazowaumiza? (b) Je, Serikali inavisaidiaje vikundi vya Beach Mananagement Unit vinavyojihusisha kuona faida ya kazi wazofanya?

Supplementary Question 1

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili wale vijana wanaoishi kando kando wa ziwa waweze kuona umuhimu wa kutunza ziwa lao na kuzuia uvuvi haramu. Ni lini sasa Serikali itaweza kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia kujenga mabwawa kando kando ya ziwa pamoja na cage ziwani ili ziweze kuwasaidi hao vijana katika kujipatia kipato ili waweze kuona umuhimu wa kutunza ziwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kila moja amekuwa akishuhudia akina mama wengi wanao nunua samaki wakiwa wamenyanganywa kwenye madishi yao, hata wale waliokaanga samaki wao wanaouza sokoni ambayo hii kusema kweli wao si wavuvi, lakini wanakuja kunyang’anywa samaki wale ambao wameshawanunua. Waziri anatoa kauli gani kuhusiana na unyanyasaji huu ambao unandelea katika baadhi ya maeneo?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, mkakati wa Serikali tulionao wa kuhakikisha tunapunguza nguvu ya uvuvi katika maziwa na kuepusha vijana na uvuvi haramu katika kuhamasisha kufanya ufugaji wa samaki; tunaomkakati sana. Hivi sasa ninavyozungumza, tumeshaanza mkakati huo katika Ziwa Victoria ambapo wako watu binafsi walioanza ufugaji wa samaki katika vizimba lakini vilevile na sisi kama Serikali tumejiandaa kuhakikisha tunatengeneza incubators, kwa maana ya vikundi vya vijana ambavyo vitakwenda kufanya shughuli ya utengenezaji wa mabwawa lakini vilevile utengenezaji wa cages kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Manyinyi ahakikishe anawaunganisha vijana wake kama nilivyotangulia kujibu katika swali la awali, wakae katika vikundi vya ushirika, nasi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tuko tayari kwenda kutoa elimu, lakini vilevile utaalam na kuhakikisha tunawasaidia vijana hawa kuwaongoza katika kufikia lengo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni juu ya kauli gani tunatoa kwa ajili ya wale akina mama na wanawake wanaouza samaki katika mabeseni. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunalinda rasilimali za uvuvi. Katika lengo hilo, hatuko tayari kuona mwanamama anayefanya biashara ya uuzaji wa samaki katika mabeseni huko masokoni, anaonewa. Kama yuko Afisa wa Serikali anayekwenda kumsumbua na kumnyanyasa mwanamke anayeuza mafungu yake matatu, manne sokoni ya samaki, hii leo natoa kauli hapa katika Bunge hili Tukufu, jambo hilo ni marufuku. Kwa sababu lengo letu siyo kuangalia hawa samaki wanaowekwa katika mabeseni, lengo letu ni kutazama hasa kiini cha makosa haya yanayotokana na uvunjaji wa Sheria ya Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niwahakikishie tu akinamama wanaouza samaki nchini kote, wawe huru katika uuzaji wa samaki wao, wahakikishe kuwa wanapata kipato cha familia zao na kujenga Taifa letu.

Name

Dr. Tulia Ackson

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Uvuvi haramu bado unaendelea licha ya adhabu kubwa inayotolewa kwa watu wamaojihusisha nao. (a) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwasaidia wananchi wake fursa zilizopo badala ya kutoa adhabu kali zinazowaumiza? (b) Je, Serikali inavisaidiaje vikundi vya Beach Mananagement Unit vinavyojihusisha kuona faida ya kazi wazofanya?

Supplementary Question 2

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nimeletewa ujumbe hapa. Siyo utaratibu, utusaidie kuzungumza lile katazo lako, wale waliokuwa wamenyang’anywa majenereta na taa zao za solar watarejeshewa ama utaratibu utakuwaje?

Majibu Mheshimiwa Waziri.

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba nimeruhusu matumizi hayo ya generator, taa za solar na wananchi wote ambao wameshikiwa zana hizo, warudishiwe bila masharti yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nilikuwa nataka kusisitiza katika hili jambo la kwamba suala la ulinzi wa rasilimali zetu hizi ni suala ambalo linahitaji kuungwa mkono na wananchi wote. Rasilimali hizi tulizonazo hapa nchini asilimia 37 ni maji, lakini mazao yetu ya uvuvi mengi yameharibiwa sana na suala la uvuvi haramu. Kwa hiyo, wananchi wote wanawajibika kuziangalia hizi sheria na kuziheshimu. Kwa sababu hata huyo Mama Ntilie anajua samaki wasioruhusiwa. Tukitengeneza mtandao huu wa huyu mama mdogo anaweza kuingia kwenye soko na samaki wasioruhusiwa, tutatengeneza mtandao ambao utawezesha kuwepo kwa soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nawaomba sana, katika kipindi hiki kigumu cha
kubadilisha watu kuwaondoa kwenye uvuvi haramu, mtuvumilie. Kwa sababu hata huyo mama mjane tunayemhurumia leo, kesho hatapata samaki wa kuuza. Hata mama mjane, mtoto yatima, watoto hawaendi shule; hawataenda shule kabisa kwa sababu samaki hawatakuwepo majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kipindi hiki ambacho tunafanya transformation hizi kubwa, nakuomba sana na bunge lako Tukufu mtuvumilie kwa nia nje kwa sababu hatua hizi zote tunazochukua ni kwa ajili ya
Taifa letu na hatima ya uchumi wa nchi hii.