Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:- Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi linazidi kuwa janga la Kitaifa nchini huku jitihada za kulikabili zikionekana kutopewa kipaumbele; hali ni mbaya katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambapo idadi kubwa ya watoto hao hujihusisha na kuomba pamoja na matukio ya uhalifu ikiwemo wizi wa vifaa vya magari kwenye maegesho. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ya kukabiliana na tatizo hili kwa nchi nzima ikiwemo kuwaweka kwenye vituo maalum na kuwapatia huduma za msingi? (b) Je, Serikali inatambua idadi kamili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa nchi nzima?

Supplementary Question 1

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa takwimu zinaonesha miji mikubwa nchini inaongoza kwa idadi kubwa ya kuwa na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ili kuwalinda watoto hawa na kuhakikisha wako katika mazingira salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa chanzo kikuu cha watoto wanaoishi mitaani ni njaa katika familia na kukosekana kwa maadili mazuri katika jamii: Je, Serikali ina mpango gani wa kukazia sheria zetu na kuhakikisha kwamba wazazi na walezi wanawajibika katika malezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo amekuwa anafuatilia kuhakikisha kwamba watoto wa Tanzania wanapata haki na ustawi ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, sisi kama Wizara tulianza katika hatua ya awali kwa kufanya tathmini ya ukubwa wa tatizo ndani ya nchi yetu na kwa kupitia mpango mkakati ambao nimeuelezea wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, tumeanza sasa kazi ya kwenda hatua ya pili ya kuanza kuwaunganisha wale watoto ambao tuliweza kuwabaini wanaishi mtaani na baadhi ya familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumekuwa tunaendeleza kampeni ndani ya mikoa mbalimbali ya kuweza kuwatambua watoto hawa na kuwarudisha katika maeneo yao ya makazi, lakini vilevile kuendelea kutoa elimu kwenye jamii kuhusiana na masuala ya matunzo ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kukazia sheria; tuna Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria hii imeweka msisitizo wa haki za msingi za watoto ambazo ningependa Bunge lako Tukufu nalo lizifahamu. Watoto wana haki takribani tano ambazo zimeainishwa kisheria; mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kutunzwa, ana haki ya kuendelezwa, ana haki ya kushirikishwa katika maamuzi yanayomhusu na mtoto ana haki ya kutobaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria hii, haki za mtoto zimeainishwa vizuri sana. Kikubwa ambacho sisi kama Wizara tunaendelea kusisitiza ni kuweka misingi ya kuwasisitiza wazazi kuhakikisha kwamba wanazingatia misingi hii ya haki za watoto na kuimarisha misingi ya familia.