Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, ni lini Serikali italeta mabadiliko katika sheria inayosimamia malipo ya fidia kwa askari anayejeruhiwa au kupoteza maisha akiwa anatekeleza majukumu ya kulinda usalama ndani au nje ya nchi kwenye vyombo vya UN au SADC Mission ili kuendana na mabadiliko ya kupanda kwa gharama za maisha?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali inajiridhisha vipi kwamba ile fidia ya dola 70,000 inayotolewa inawafikia walengwa hasa watoto au mke wa marehemu ambaye anakuwa amepoteza maisha anapokuwa katika vikosi vyetu vya kulinda amani nchi mbalimbali huko duniani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni muda mrefu sasa tunaendesha mambo yetu ya ulinzi bila kuwa na sera ya ulinzi, je, ni lini Serikali itakamilisha sera hii ili kusudi pamoja na masuala haya ya ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani. Sera hiyo iweze kubainisha maeneo mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yatafanya vikosi vyetu vinavyoenda kulinda amani huko duniani viweze sio tu kunufaika kwa mujibu wa taratibu za UN, lakini pia kwa mujibu wa taratibu za nchi yetu? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, fedha zinazotolewa kama fidia zinawafikia wahusika kwa sababu Tanzania tumeshakuwa na uzoefu wa jambo hili, tumeshapoteza askari wetu na kuna walioumia, fedha zilizotolewa familia zinaitwa Makao Makuu ya Jeshi na wanakabidhiwa bila ya tatizo lolote na inapobidi basi msimamizi wa mirathi ndiye ambaye anakabidhiwa akiwa pale Makao Makuu ya Jeshi. Mpaka sasa hivi kwa matukio yote yaliyotukuta hakuna tatizo la mtu kudhulumiwa na hivyo tunaamini kwamba fedha hizo huwa zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ya Sera ya Ulinzi, kama tulivyowahi kusema mara kadhaa hapa Bungeni, sera hii rasimu yake ipo tayari, imeshajadiliwa na ngazi zote na kinachosubiriwa ni maoni kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama mdau ili wakishatoa maoni yao basi hatua zilizobaki za kuikamilisha sera hii ziweze kuchukuliwa.

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, ni lini Serikali italeta mabadiliko katika sheria inayosimamia malipo ya fidia kwa askari anayejeruhiwa au kupoteza maisha akiwa anatekeleza majukumu ya kulinda usalama ndani au nje ya nchi kwenye vyombo vya UN au SADC Mission ili kuendana na mabadiliko ya kupanda kwa gharama za maisha?

Supplementary Question 2

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupana nafasi, Mheshimiwa Waziri amesema kama askari au afisa amefariki analipwa dola 70,000. Sasa ningependa kujua dola 70,000 hizi wanalipwa warithi wake cash au kuna mgao wa Serikali unakatwa kutoka hizi kama ambavyo wanakatwa wale askari wanaoenda katika misheni zile, sijui umenielewa?

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, fedha hizi hazikatwi, wanapewa dola 70,000 zote lakini sio mwisho, hii ni fidia kutoka Umoja wa Mataifa lakini askari yeyote anayepoteza maisha ana fidia vilevile kutoka hapa nyumbani. Kwa hiyo, kuna fedha zinazotolewa na Wizara kwa ajili ya kulipa fidia familia ya wale ambao wamepoteza maisha wakiwa kazini.